Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameagana na Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Dany Kazungu ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na balozi Kazungu Waziri Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji kazi uliotukuka wa Balozi Kazungu ambao umewezesha Tanzania na Kenya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu, kijirani na kijamii ambao umekuwepo siku zote.
Amesema uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Kenya ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa balozi Kazungu nchini na kuchochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na ustawi wa jamii katika nchi hizo na amemuomba Balozi huyo kuwa balozi mzuri wa Tanzania pindi atakaporejea nyumbani kwao Kenya.
“Katika kipindi chako cha uwakilishi umeiwakilisha vyema Kenya hapa nchini na kuonesha mafanikio makubwa ambayo Tanzania na Kenya tumeyapata kwa pamoja, kazi yako imechochea ukuaji wa biashara uwekezaji na hata ustawi wa jamii katika nchi zetu, nikuombe ukawe balozi mzuri wa Tanzania nchini Kenya’, alisema Mhe. Waziri.
Naye Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Dany Kazungu amesema anajivunia uwepo wake hapa nchini, amejifunza mengi ikiwemo kuthamini utu na ukarimu wa Watanzania, na amewashukuru Watanzania kwa upendo mkubwa waliomuonesha katika kipindi cha miaka minne aliyokuwepo nchini.
“shukurani nyingi kwa upendo wenu Watanzania, mhe. Waziri niwaombee heri na baraka zote katika harakati za kuijenga Tanzania, ni wakati mgumu kusema kwaheri lakini hakuna budi, tuendeee kushirikiana na tufanye kazi pamoja ili kuleta mendeleo ya watu wetu, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania, mnathamini utu hakuna kukwezana, nimmejifunza hili toka kwenu” alisema Mhe. balozi Kazungu
Amesema daima atakumbuka tabia ya Watanzania kutokutweza utu wa mtu na ukarimu wao na kuahidi kuwa atakuwa balozi mwema wa Tanzania nchini Kenya na kuwaombea heri na baraka katika hatau mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikizichukua chini ya Uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan.
0 comments:
Post a Comment