METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 26, 2022

MAJALIWA: WATANZANIA TUSHIKAMANE KUIPA THAMANI TANZANITE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watanzania kushirikiana na kushikamana ili kuyapa thamani madini ya Tanzanite na kuifanya dunia nzima itambue kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania tu na tayari imeweka mazingira ya kuyaongezea thamani.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 26, 2022) alipozungumza na wananchi katika eneo la EPZA unapojengwa Mji wa Tanzanie katika Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Manyara.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itahakikisha rasilimali zote zilizoko nchini yakiwemo madini ya Tanzanite zinawanufaisha wananchi wote hususani wanaoishi katika maeneo zinapopatikana. “Watanzania lazima tushirikiane na tushikamane kuyapa thamani madini hayo.”

Amesema kuwa Serikali itaendelea kukutana na wafanyabiashara wa sekta madini kwa lengo la kuhakikisha kwa pamoja wanaweka mikakati ya kusaidia kuikuza sekta hiyo ili iendelee kuleta tija kwa watanzania na taifa kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kukagua eneo la uwekezaji la EPZA, Waziri Mkuu amewataka watanzania kujitokeza na kuwekeza katika eneo hilo “Watanzania tumieni fursa ya eneo hili kuwekeza mtakapa faida”

Mheshimiwa Majaliwa aliwasisitiza wananchi waendelee kufanya biashara hiyo ambayo ina manufaa makubwa kwao na Taifa kwa ujumla na kwamba Serikali ipo tayari kuwahudumia wakati wote. “Tumejipanga kuwahudumia iwe wakati wa jua au wakati wa mvua.”

Naye, Naibu Waziri Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amemuahidi Waziri Mkuu kuwa watahakikisha wanasimamia ujenzi wa eneo hilo ili liweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa watanzania wenye nia ya kuwekeza.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea na alikagua soko la madini ya Tanzanite la Tanzanite Forever Lapidary ambapo alishuhudia hatua mbalimbali za uchenjuaji wa madini hayo pamoja na namna biashara hiyo inavyofanyika kwa njia ya uwazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzanite Forever Lapidary, Faisal Juma Shahbhai alisema licha ya maboresho yaliyofanyika katika sekta ya madini, pia ameishauri Serikali iweke mipango mahsusi itakayolinufaisha zaidi Taifa kiuchumi kutokana na uwepo wa madini hayo.

“Sasa biashara inafanyika kwa urahisi, sisi wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite tunaridhishwa na utendaji kazi wa Serikali kwani tupo katika mfumo mzuri sana. Naishauri Serikali ihakikishe wafanyabiashara wanakua specific ili tuyatendee haki madini haya.”

Pia ameishukuru serikali kwa uamuzi wa kuelekeza biashara ya madini ya tanzanite ifanyike katika eneo la mirerani yanakopatikana madini hayo kwa sababu imewezesha wakazi wa maeneo hayo kunufaika.

Naye, Kaimu Afisa Madini Mkazi, Mirerani Fabian Mshai amesema tangu kuboreshwa kwa kanuni ili kuruhusu buiashara na uongezaji thamani madini ya Tanzanite kufanyika Mirerani hadi sasa jumla ya wafanyabiashara wakubwa wa madini 48 wananunua madini hayo na kuyachakata kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini hayo.

“Tangu kuanzishwa kwa biashara na uongezaji wa thamani wa madini ya Tanzanite Mirerani, mpaka sasa jumla ya Vibali 105 vya usafirishaji wa madini hayo nje ya nchi vimetolewa kwenda nchini India, Ujerumani, China, Marekani, Thailand, Uingerea, Uhispania na Uswisi”

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com