

Na Innocent Natai
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rombo Ndg. Antony Tesha amewataka vijana wa Wilaya hiyo kutumia vyema muda wao kwa kushiriki mashindano ya Rombo Samia Football Friendship Tournament kwani yatawasaidia kuimarisha afya, kukuza vipaji vyao na kuwaepusha na vitendo visivyo na maadili
Tesha ameyasema hayo hivi leo 24 Julai,2022 katika viwanja vya Saba Saba Wilayani hapo wakati akifungua mashindano wa mpira wa miguu yatakayo shirikisha timu za kata zote za wilaya hiyo yaliyopewa jina la Rombo Samia Football Triendship Tournament yakilenga kutangaza shughuli lukuki zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Profesa Adolf Mkenda ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo,toka kuchaguliwa kwao.
Aidha amempongeza Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Profesa Adolf Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia kwa ubunifu mkubwa wa kuandaa mashindano mbalimbali katika jimbo hilo ambayo yanalenga kuwaepusha vijana na makundi yasiyofaa na kuwaimarisha kiafya
Ameongeza; "mimi kama mwenyekiti wa CCM wilaya hii naahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mbunge kwa kuhakikisha mashindano haya aliyoyaandaa yanafanikiwa na tunatangaza makubwa yaliyofanywa na Mhe. Rais na kila mwaka tutaunga mkono jitihada hizi, ," Ndg. Antony Tesha
Aidha amewataka wadau wa maendeleo wilayani humo kujitokeza na kuunga mkono jitihada za kuendeleza michezo wilayani humo ili kuhakikisha vijana wa Wilaya hiyo wanapata fursa ya kimichezo na kuendeleza vipaji vyao
"Ndugu zangu michezo ni ajira, tukiendeleza tasnia ya michezo katika wilaya hii vijana mtapata ajira na ndio maana leo hii tunaona Mbunge wetu Mhe. Profesa Adolf Mkenda mbali na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kwenye jimbo letu ameamua kuinua michezo kwa kuandaa matamasha ya michezo ya mara kwa mara," amesema Ndg. Antony Tesha
Naye Mwenyekiti wa UVCCM wilaya hiyo, John Kanyau amesema baada ya uzinduzi wa bonanza hilo la michezo wilayani humo wataanza kucheza kwa ngazi za kata na mashina ili kumpata bingwa wa Wilaya.
0 comments:
Post a Comment