Na Mathias Canal, Wizara
ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda leo tarehe 1 Disemba 2021
amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Bia cha Tanzaia
Breweries Limited-TBL Ndg Jose Moran katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo
Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkenda ameipongeza TBL kwa kazi wanayoifanya nchini ikiwemo
kutoa mikataba 4000 kwa wakulima wa mtama wilayani Kongwa katika mkoa wa Dodoma
ambapo wamenunua mtama wa wakulima Tani 10,000.
“Utaratibu huo unawasaidia wakulima kwani hata mkulima mdogo
anaweza kuingia kwenye kilimo cha kibishara kwenye mazao ya chakula kwahiyo na
sisi kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inapaswa kutumia utaratibu
huo unaofanywa na TBL kwa wakulima, tena wafanye hivyo Wilayani Kongwa na
kwingineko nchini kwa kuwa soko la Mtama limepatikana nchini Sudani Kusini”
Amekaririwa Prof Mkenda
Waziri Mkenda amebainisha kuwa pamoja na mkataba wao kuwekwa
lakini amemuomba mkurugenzi huyo wa TBL kuhakikisha kuwa ananunua mtama mwingi zaidi
kwa wakulima.
Kuhusu zao la shairi ambalo TBL wana mkataba na wakulima 400
katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilayani Karatu ambapo mpaka sasa wamenunua Tani 5000, Waziri Mkenda amefanya mazungumzo
na Mtendaji Mkuu wa TBL ili kuona uwezekano wa kununua Shairi kwa wakulima
kwani walizasha kiasi kikubwa kuliko kilichoainishwa kwenye mkataba.
Kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu baina ya serikali na
wazalishaji wa Bia nchini kuhakikisha kuwa wanatumia shairi inayolimwa nchini
kwa ajili ya kutengeneza kimea ili wanywaji wa Bia wachangie mapato ya mkulima,
Kodi na kuunda ajira kwa wananchi.
Waziri Mkenda amesema kuwa mazingira ya kikodi kwa wazalishaji wa
Bia nchini kwa sasa ni mazuri hivyo ujenzi wa kiwanda cha Kimea kikijengwa
kitaongeza soko la shairi kwa wakulima kutoka kwenye mkataba wa ununuzi wa Tani
5000 za shairi mpaka Tani 35,000
“Unajua kila unapokunywa Bia nchini unakuwa umepeleka ajira nje ya
nchi, unapeleka kodi kwa serikali ya nje na kupeleka fedha kwa wakulima wa nje ya
nchi, Hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na kiwanda cha Kimea
hapa hapa nchini” Amesisitiza Waziri Mkenda
Prof Mkenda amesema kuwa hiyo itakuwa hatua kubwa ya kuwainua
wakulima wengi watakaojihusisha na kilimo hicho nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuno ya Bia (TBL) Ndg Jose
Moran amemueleza mwenyeki wake ambaye ni Waziri wa Kilimo kuhusu Maendeleo ya Mkakati
wa kuanza ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza Kimea kwani kimea kinachotumika
nchini kinaagizwa nje ya nchi.
Mkurugenzi wa TBL amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa kati ya mwisho wa mwezi Januari, Februari mpaka Machi watakuwa tayari na tangazo linaloeleza ni lini shughuli ya ujenzi itaanza mwakani.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment