METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 3, 2021

MTANDAO WA BARABARA SINGIDA WABORESHA MAISHA YAWANANCHI


Na Hamis Hussein - Singida 










Mkoa wa singida umetajwa kuwa na mtandao mkubwa  ya barabara wenye urefu wa jumla ya  kilometa 1716.12  ambapo lami ni   Km 488.73 na changarawe ni  km  1,227.39 . 
uwepo wa mtandao wa barabara kuu na za zile zinazounganisha mkoani Singida umeongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi na kukuza uchumi wa mtu mmoja moja kutokana na biashara zinazofanyika baina ya wilaya na halmashauri mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akifungua kikao kazi cha 44 cha Bodi ya barabara ya Mkoa  ambacho kimefanyika  Desemba 3, 2021 katika ukumbi wa mkoa huo  na kuhusisha wakala wa barabara (TANROAD), Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wabunge wa mkoa huo, Viongozi wa CCM mkoa, wenyeviti wa Halmashauri, wakurungezi watendaji, na wataalamu mbalimbali wa Serikali.

Dkt Mahenge alisema mifumo ya barabara iliyopo katika Mkoa huo imefungua fursa mbalimbali  za kiuchumi kwa kuwa imeendelea kuunganisha Mkoa na Mikoa mingine, miji na  maeneo ya kitalii pamoja na migodi ya madini.

“Mifumo ya barabara imekuwa kama mishipa ya damu ambayo ikisimama kila kitu kina simama, nawashukuru sana TANROAD na TARURA kwa kusaidia kuboresha barabara za lami na zile zenye kiwango cha changarawe” alisema RC. Mahenge.

katika Kikao hicho ambacho kililenga kupitia miradi mbalimbali ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 RC mahenge akatumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi waliohudhuria kikao hicho kuhakikisha wanasaidia kusimamia ujenzi wa barabara zote zinazoendelea  katika maeneo mbalimbali mkoani hapo kwa kuwa fedha nyingi za barabara zinaendelea kuja.

Aidha Mkuu wa Mkoa akaendelea kuwakumbusha wakandarasi wote wanaoshughulika ujenzi wa barabara  kuhakikisha wanatekeleza kazi zao kwa muda walipewa kwa kuwa hatapenda kusikia sababu zozote zitakazosimamisha ujenzi huo.

Akiwakilisha taaraifa ya Utekelezaji wa miradi ya barabara  Meneja wa TANROAD Mkoa Mhandshi Erick Ng’walali amesema hali ya barabara  katika Mkoa wa Singida  inaridhisha  kwa kuwa  asilimia 63.1 ni barabara zenye hali nzuri, asilimia 27.6 ni hali ya wastani wakati asilimia 9.3 tu zina hali  mbaya.

Mhandisi Erick akafafanua kwamba bado wameendelea kufanya matengenezo katika baadhi ya barabara mkoani hapo  ambapo asilimia 32.7 zimekamilika  na asilimia 14.4 za fedha zimekwisha tumika.

Hata hivyo Mhandisi Erick akazitaja baadhi ya changamoto zikiwemo wizi wa vyuma na alama za barabarani ambapo amesema elimu na uhamasishaji vinahitajika katika maeneo mbalimbali ili kutunza alama hizo ambazo ni muhimu kwa watumiaji wa barabara huku akiwaonya baadhi ya watu wanaotumia vibaya hifadhi ya barabara ikiwemo kupasua mifereji ya maji, kujenga na kupitisha mifugo katika sehemu ambazo hazistahili.

Akitoa maadhimio ya kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amesema ahadi zote zilizotolewa na viongozi wa juu kuhusiana na ukarabati na utengenezwaji wa barabara utaingizwa kwenye mpango na kuhakikisha  unatekelezwa na wananchi wanafaidika.

Aidha amewataka TANROAD na TARURA kuboresha barabara na madaraja yote yenye uhitaji huo ndani ya mkoa mzima ili kuondoa athari zinazoweza kutokea wakati wa mvua.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com