METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 22, 2021

KIGOMA YAZINDUA MPANGO KAZI KUTOKOMEZA UKATILI WA WANAWAKE NA WATOTO

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta akizungumza  na washiriki wa Kongamano la siku mbili la kupinga ukatili wa Wanawake na Watoto kabla ya kuzindua Mpango kazi wa Mkoa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

 Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mpango kazi wa Mkoa wa Kigoma wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Grace Mwangwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza akieleza umuhimu wa mpango kazi wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto mkoa wa Kigoma kabla ya uzinduzi wa mpango kazi huo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Grace Mwangwa akiwasilisha Mpango kazi wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa wadau wa Mkoa wa Kigoma wenye Kaulimbiu Twende Pamoja Ukatili Kigoma sasa basi.

 

Sehemu ya washiriki ni wadau wa Mkoa wa Kigoma walioandaa Mpango kazi wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto wakifuatilia uzinduzi wake uliofanywa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta.

Na WAMJW, Kigoma

Mkoa wa Kigoma umezindua Mpango kazi kuhakikisha vitendo vya  ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto vinatokomezwa na kuondoa nafasi ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo.

Akizindua Mpango kazi huo Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Rashid Mchatta amesema atasimamia Halmashauri kuhakikisha zinatenga bajeti kutekeleza mkakati huo kwani ni wajibu wa kila mmoja kuweka juhudi na jamii kuwa na uelewa kuhusu madhara ya vitendo hivyo.

“Yote ambayo yameazimiwa katika Mpango huu yatatekelezwa na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kutokomeza vitendo hivyo. Ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake awajibike baada ya kutoka hapa na tutakuwa tumewatendea haki wanawake na watoto. Suala la lishe na hili la ukatili wa watoto na wanawake tutayatilia mkazo” alisema Mchatta.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka ya Afya Mwajuma Magwiza amesema Mpango kazi huo utaendeleza kwa kasi Kampeni hiyo ya Twende pamoja ukatili sasa basi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

“Suala hili siyo la kuiachia Serikali ila wanajamii na wadau sote kwa pamoja tuungane mkono juhudi hizi kwa ajili ya kuweka bajeti zetu ambazo zote zitaelekeza nguvu katika kupambana na ukatili uliopo Mkoani Kigoma na Tanzania nzima” alisema Magwiza.

Aidha, Magwiza amehimiza Jamii ishirikishwe katika utekelezaji wa mpango huu na kupata taarifa katika kila hatua inayofikiwa.

Akiwasilisha Mpango kazi huo Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Grace Mwangwa ameikumbusha jamii kutekeleza wajibu wao kulingana na nafasi zao na kusema kuwa Mpango umejumuisha masuala mbalimbali yaliyoainishwa na Wadau katika kongamano lililofanyika awali.

Grace amesisitiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake kwenye Mamlaka ili hatua zichukuliwe kwa wanaofanya vitendo hivyo.

“Ukatili mwingi unaanzia ndani ya familia, kwa sababu vitendo vinapotokea wanaamua kuyamaliza nyumbani hali inayopelekea ukatili kuongezeka kwani wanaofanya vitendo hivyo wanakuwa hawajachukuliwa hatua” amesema Grace.

Kwa upande wake mmoja wa Viongozi wa dini aliyeshiriki katika uzinduzi huo Shekh Rashid Haruna Hamis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya MTAKUWWA katika Kata ya Gungu, Kigoma Ujiji amesema kuwa Serikali inafanya vema kushirikiana na Wadau wote katika kukemea vitendo vya ukatili, akitaja mmomonyoko wa maadili ni chanzo kikubwa kusababisha vitendo hivyo.

Baadhi ya wananchi na Wadau walioshiriki kuandaa Mpango kazi huo baada ya majadiliano ya kina, akiwemo Beatrice Mtesigwa na Gervas Lwako wamesema mitandao ya kijamii ni changamoto kwa kwa kizazi cha sasa na kuomba Mamlaka zinazohusika kuhakikisha kesi za vitendo hivyo zinafanyiwa kazi haraka.
 
Mpango kazi huo imeandaliwa kwa pamoja na wadau mbalimbali wa Mkoa huo walioshiriki kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kujadili namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili mkoani hapo na kukubaliana Kaulimbiu ya Mpango huo ni Twende Pamoja, Ukatili Kigoma sasa basi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com