METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, December 20, 2021

DKT MABULA: TUMPONGEZE RAIS SAMIA KUWEKA USAWA WA KIJINSIA

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka taasisi ya Zawadi Initiativi(hawapo pichani)  

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akimkabidhi cheti moja ya wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kutoa taasisi isiyo ya serikali ya zawadi initiative 

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na taasisi ya Zawadi Initiative

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa kuhitimisha mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko kata ya Mecco wilaya ya Ilemela katika ukumbi wa Mtena ‘B’ Buzuruga ambapo amefafanua kuwa jamii haiwezi kuwa na kizazi chenye usawa kama hakuna chombo kinachosimamia suala hilo kwani kumekuwepo na vyombo na majukwaa mbalimbali ya kupigania usawa lakini yameshindwa kufikia malengo hivyo kitendo cha Rais Mhe Samia Suluhu Hasan cha kukusudia kutengenisha wizara ya afya na maendeleo ya jamii kuwa wizara mbili tofauti ni cha kuungwa mkono na kupongezwa kwani kitaongeza kasi ya usimamizi wa masuala hayo pia kitasaidia kufikia lengo la kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kuwakomboa wanawake kiuchumi

‘.. Kutenganisha wizara hii ni jambo linaloenda kuweka mabadiliko chanya, Tutaenda kuona kasi ya maendeleo kwa kugusa jinsia zote katika utendaji, Tunapozungumzia masuala ya uwezeshaji kiuchumi na kuleta usawa wa kijinsia maanake sasa tutakuwa tumeyagusa makundi yote lakini anaelengwa zaidi ni mwanamke ambae kidogo amekuwa nyuma katika mambo mengi..’ Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula ameongeza kuwa Serikali ya Rais Samia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kumkomboa mwanamke ikiwemo kuendelea kutoa elimu bila malipo, kutoa fursa kwa mabinti watakaopata ujauzito kwa bahati mbaya kuendelea na shule kama sheria na sera itakavyoelekeza, pamoja na kufuta tozo zaidi ya 108 zilizokuwa kero katika masuala ya umiliki wa ardhi na nyanja nyenginezo

Kwa upande wake afisa maendeleo wa manispaa ya Ilemela Ndugu Sitta Singibala amewataka wahitimu hao kutobweteka na elimu waliyoipata badala yake wajiunge katika vikundi ili waweze kukopesheka na kujikwamua kiuchumi huku Diwani wa kata ya Buzuruga Mhe Manusura Sadick akiwahakikishia ushirikiano katika kuhakikisha wanakuwa na mazingira rafiki ya kujiajiri na kujiletea maendeleo

Akihitimisha mratibu wa mpango huo kutoka kituo cha Zawadi Yangu Initiative Bwana Atiupele Amon Mwakitalu amesema kuwa mafunzo hayo yametolwa bure bila gharama zozote na jumla ya mabinti 44 wamehitimu mafunzo hayo huku 12 wakishindwa kufuzu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito na umbali kutoka makazi wanayoishi.

Grace Jeremiah ni moja ya wahitimu wa mafunzo hayo ameishukuru taasisi ya Zawadi Initiative kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwani yatawasaidia katika kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira pamoja na kuleta ushindani katika soko.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com