Na.WAMJW DODOMA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta na Wakuu wa Mikoa na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali hapa nchini kuhakikisha wanajenga uwezo kwa watendaji ngazi ya Halmashauri na Wilaya ili kuwezesha ufanisi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kwa lengo la kukabiliana changamoto ya makuzi ya watoto chini ya miaka nane ikiwemo idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao hupoteza maisha kutokana na matatizo yanayohusiana na lishe duni kila mwaka hapa nchini.
Akitoa wito huo wakati akihutubia kwenye uzinduzi wa programu ya kihistoria, ya kwanza Afrika Mashariki na Kati. kwa maendeleo ya watoto wakati alimuwakilisha Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ambaye yupo kwenye majukumu mengine ya kitaifa katika hafla ilifanyika leo desemba 3.
Uzinduzi wa program hiyo umeshuhudiwa na Mawaziri, Waganga wakuu wa Wilaya, Maafisa Ustawi wa Jamii, Waandishi wa Habari Wabobezi, Makundi Maalum ya Watoto, Mashirika ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani ( WHO ), Benki ya Duniani na Asasi zisizokuwa za Kiserikali.
DKt Gwajima amesema kuwa wazazi na walezi kutokuwa karibu na watoto kunachangiwa kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa uelewa wa kina kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambapo takwimu za mwaka 2018 zilibaini zaidi ya watoto 2,600,000 chini ya mika mitano wamedumaa na kwamba asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji na maendeleo yao kutokana na viashiria mbalimbali vikiwemo utapiamlo, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa mawazo katika familia, miundombinu duni katika familia, uhaba wa rasilimali pamoja na utelekezaji na unyanyasaji wa watoto.
Dkt Gwajima amesema kuwa ili kukabiliana na hali hiyo Serikali inatarajia kujenga vituo vya mfano vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kila kijiji/mtaa na kwenye shule za msingi nchi nzima ili kupunguza ukatili na udumavu kwa watoto ambapo Serikali na Wadau inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kipindi cha 2017/18-2021/22. Pamoja na hayo, mwaka 2017, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kutenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa kila mtoto kuwezesha kutekeleza afua za kutokomeza udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano.
"Ukatili dhidi ya Mtoto bado ni changamoto kubwa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Taarifa ya Ukatili wa Kijinsia wa Jeshi la Polisi nchini inaonyesha katika mwaka mmoja uliopita matukio yameongezeka kutoka 15,680 kwa mwaka 2019 hadi matukio 15,870 kwa mwaka 2020. Katika kipindi cha miezi 9 kuanzia Januari hadi Septemba, 2021 jumla ya matukio 6,168 wakiwemo yanayowahusu wasichana 5,287 na wavulana 881 yalitolewa taarifa katika vituo vya polisi. Haya ni matukio yaliyotolewa taarifa tu, lakini naamini kuna matukio mengi ambayo hayatolewi taarifa zake Polisi " alisema Dkt Gwajima
Programu hiyo ambayo itakuwa chini ya uratibu wa Kisekta kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaliwa na Wizara ya Afya na Wadau wote wakiwemo Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha na Mipango ambapo kwa pamoja wametoa matamko mbalimbali yenye lengo la kunusuru maisha ya watoto. Wizara ya mambo ya ndani kupitia Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia imetoa tamko kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kudhibiti masuala ya unyanyasaji kwa ajili ya kuwezesha watoto kuwa salama wakati wote na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa wanaohusika na nyanyasaji, ukatili na uzalilishaji wa watoto wadogo. Amesema Naibu waziri ya Mambo ya ndani ya Nchi Mhe Hamis Hamza Chilo.
0 comments:
Post a Comment