METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 23, 2021

WAZIRI MKENDA AWASILI NCHINI UGANDA KWA AJILI YA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU NNE








 Na Mathias Canal, Entebbe-Uganda

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 23 Novemba 2021 amewasili Mjini Entebbe nchini Uganda kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia tarehe 23 Novemba 2021 mpaka tarehe 26 Novemba 2021 ambapo atapata fursa ya kujifunza mafanikio ya Kilimo bora cha Michikichi.

Ziara hiyo ni mualiko wa kampuni ya Wilmar Internation kwa ajili ya kwenda kujifunza kilimo cha Michikichi nchini Uganda kwa utaratibu wa (Block Farming) unaowaunganisha wakulima na viwanda vya kukamua mafuta ya kula ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano na kampuni hiyo na Wizara ya Kilimo mara baada ya kukutana kwenye vikao kazi nchini Tanzania vilivyojadili namna Kampuni hiyo inavyoweza kuwekeza kwenye tasnia za mazao ya mafuta ya kula ikiwemo michikichi, alizeti na maharage ya soya.

Katika ziara hiyo Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye, Mkurugenzi wa Maendeleo Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu na wataalam wengine wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Waziri Mkenda atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda Mhe. Frank Kagyigyi Tumwebaze, kadhalika atafanya ziara kwenye kiwanda cha kampuni ya Wilmar International ambayo imeonyesha nia kuwekeza kiwanda cha mafuta ya kula kwa ubora wa mwisho kutokana na uzalishaji wa michikichi, alizeti na maharage ya soya nchini Tanzania.

Waziri Mkenda amesema kuwa ili uwekezaji huo uwe na tija uhakika wa malighafi ni suala muhimu ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo bora wa uzalisaji kama vile mashamba makubwa (Block Farming) yanayowahusisha wakulima wadogo.

Amebainisha kuwa kwa upande wa Michikichi kampuni hiyo ingependa kuanzisha mashamba ya pamoja yenye ukubwa wa angalau ekari 10,000 kwa kila shamba.

Kampuni hiyo ya Wilmar inamiliki mashamba katika nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, Indonesia na Malaysia.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com