METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 24, 2021

TANZANIA YADHAMIRIA KUPUNGUZA UAGIZAJI WA MAFUTA NJE YA NCHI








Na Mathias Canal, Kaangala-Uganda

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema serikali imejipanga katika kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa zao la michikichi ili kuhakikisha nchi inapunguza ama kumaliza kabisa kadhia ya kuagiza mafuta ya mawese kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkenda ameyasema hayo tarehe 25 Novemba 2021 katika ziara yake nchini Uganda wakati akikagua shamba la Michikichi lililopo katika kisiwa cha Kalangala Nchini Uganda linalomilikiwa na kampuni ya Oil Parm Uganda Limited wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne nchini humo.

Waziri Mkenda amesema kuwa ziara yake nchini Uganda imelenga katika kuangalia ni kwa namna gani wamejipanga katika kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa zao la michikichi na ni kwa namna gani serikali ya nchi hiyo inavyojipanga kuhakikisha mwekezaji wa shamba hilo anaweza kufanya kilimo hicho na kikawanufaisha wananchi wanaolizunguka shamba hilo na wao kuwa na mashamba madogo madogo.

“Sababu moja ya kuja hapa kumekuwa na hadithi tunaambiwa kwamba asili ya michikichi ni Kigoma Tanzania sasa kila siku ninasema sina uhakika lakini hapa wakati tunaangalia hizi mbegu tumeona aina fulani inaitwa Tanzania lakini imetoka Kostarika kwa hiyo inamana kuwa walipochukua michikichi mbegu hizi wakapeleka Kostarika zamani hizo walibakiza lile jina la Tanzania” Amekaririwa Waziri Mkenda

Aidha, Prof Mkenda amesema kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha zao la michikichi na kuweza kupata mafuta ya mawese japo kwa sasa Tanzania inazalisha kiasi kidogo cha mafuta ya mawese, kitendo kinachosababisha serikali kutumia fedha nyinyi kuagiza kutoka nje.

Waziri Mkenda amesema kuwa kama mwekezaji akipata eneo la kuwekeza nchini Tanzania serikali itahakikisha kuwa wananchi nao wanaotesha  michikichi ili wapate fedha.

“Katika maelekezo tuliyopewa hapa tumeambiwa kwenye hekta tatu mkulima anaweza kupata milioni 30 kwa mwaka hizo ni hela nyingi kama wakulima wetu tukiweza kuhakikisha wanapata na itakuwa sio kulima tu michikichi anaweza akawa anafanya na shughuli nyingine pia” Amesema Waziri Mkenda

Ameongeza kuwa Kitu kikubwa ambacho wamekioni katika ziara hiyo ni suala la umuhimu wa utafiti ambapo amesema wameambiwa sasa hivi mbegu nzuri zinazozalishwa zaidi ni mbegu zinazotoka Benini na Afika Magharibi kwenye kituo cha utafiti kinachoendeshwa na serikali ya Ufaransa na hivyo kama serikali ni lazima utafiti uimarishwe ili kupata mbegu nzuri.

Katika ziara yake Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Naibu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Afisa Kilimo wa Kigoma, Maafisa utafiti kutoka Tanzania ambapo dhumuni la kuambatana na wataalamu hao ameeleza ni kuangalia mambo ambayo wanaweza kuyachukua ili kuyafanyia kazi watakaporejea nchini.


MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com