Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wafanyakazi majumbani na
kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu la Jijini Mwanza WOTESAWA
limefanikiwa kuwaokoa Zaidi ya watoto
900 waliokuwa wakifanya kazi za majumbani chini ya miaka 14.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari wakati wa
maadhimisho ya miaka 10 kuanzishwa kwa shirika hilo novemba 9, 2021 Mkurugenzi wa
shirika Anjela Benedicto ameyataja hayo kama sehemu ya mafanikio ya shirikia
hilo, pamoja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Mbali na mafanikio hayo amesema kupitia wafadhili
mbalimbali shirika limeweza kuwapa ujuzi watoto katika fani mbalimbali ikiwemo
utengenezaji wa nywele na kuwawezesha kufungua ofisi zao huku wengine wakipata
wafadhili kwa ajili ya kuendelea na masomo.
“watoto hawa baada ya kuwaokoa tuliwapa msaada wa
kisheria, wengine tumewawezesha kimafunzo yakiwemo ya kiuchumi mfano mafunzo ya
saluni na hivi tunavyozungumza wapo ambao wameshaacha kazi za ndani na
kuajiriwa na wengine wamefungua ofisi
zao.” Alisema
Aidha amesema bado jamii haijamthamini sana mtoto wa
kike na ndo maana matukio mbalimbali ya ukatili yanaendelea kujitokeza likiwemo
hilo la kuwatumikisha kwani baadhi ya jamii hasa akina baba kukwepa majukumu
yao ikiwemo kutunza familia hivyo mtoto wakike hutumiaka kama sehemu ya kipato
cha familia.
“Unajua hili suala sio la mtu mmoja tunapaswa
kushirikiana kwa pamoja, nasi kama Wote sawa tumekuwa tukishirikiana na taasisi
nyingine katika kuhakikisha tunawalinda hawa watoto mfano wakati Fulani
tulikutana na watoto ambao wanatoka nje ya nchi hivyo kwa kushirikiana na
mamlaka nyingine tunafanikisha kuwarejesha watoto hawa.” Aliongeza.
Akizungumzia ziara ya Balozi wa Marekani katika
kituo hicho amesema ujio wa balozi huyo ni fursa ya kipekee kwao kutembelewa na
ugeni huo ni fahari na faraja kubwa sana kwao, wakiamini kwamba ni mwanzo mzuri
wa mafanikio makubwa ya shirika hapo baadae.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi
Robert Gabriel aliyeambatana na ugeni
huo, aliitaka jamii kutokalia kimya matukio yoyote ya ukatili yanayofanyika na
hivo taarifa ziweze kutolewa ili kukomesha vitendo hivyo.
“Sisi kama Serikali tutashirikiana nae, na niwaombe
mtoe taarifa mtakapoona mtoto mwenye umri wa kwenda shule hapatiwi haki hiyo na
endapo mtaona mtoto anatumikishwa kwa namna yoyote ile basi mtoe taarifa kwa
mamlaka husika ili waweze kurejeshwa kwenye familia zao.” Alisema
Aidha amelipongeza shirika la wote sawa kwa
kushirikiana pamoja na Serikali na wanapata faraja sana kuona Mkoa unakuwa na
vituo vya makimbilio kwa watoto ambao wamekuwa wakikutana na changamoto
mbalimbali kutoka kwenye jamii.
Akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa shirika
hilo Balozi wa Marekani hapa nchini Donald Wright awali alimpongeza Mkurugenzi
wa shirikia hilo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha watoto wanapata haki
yao na kuwa na maono hayo makubwa kwa kipindi cha miaka 10.
“Nichukue nafasi hii kukupongeza Anjela kwa maono
haya makubwa ya kuhakikisha unawajengea uwezo watoto na hasa wanawake katika
Nyanja mbalimbali hasa katika kuwapatia ujuzi kupitia fani mbalimbali, najua
kuna changamoto nyingi sana katika kufanikisha hili lakini hongera kwa namna
ambavyo umelianzisha na unavyoendelea kulisimamia.” Alisema Balozi Donald
Wright
0 comments:
Post a Comment