Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekouture
imezindua kambi ya siku tano(5) iliyoanza Novemba 15 hadi Novemba 19 mwaka huu
inayohusisha madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali hapa Nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Katibu
Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg, Ngusa Samike aliupongeza
uongozi wa hospitali na madaktari kuja na mpango Mkakati wa kuhakikisha
wanawafikia wananchi wengi.
Alisema kuna changamoto kubwa sana kuwapata madaktari
Bingwa, hivyo ili kuwafikia wananchi wengi wameona kuna haja ya kuanzisha kambi
huku akibainisha kwamba wataalamu wote wamegharamiwa na serikali kupitia mapato
ya serikali.
Sambamba na hilo aliwapongeza madaktari, wauguzi na
wataalamu wote ambao wanashiriki kutoa huduma katika kipindi chote cha uwepo wa
Kambi hiyo, akisema kwamba ni moyo wa kujitolea ambao umesukumwa na moyo wa
dhati wa kuhudumia wananchi.
Akizungumzia maboresho ya hospitali hiyo alisema
wako katika ukamilishaji wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto lenye uwezo wa
kubeba vitanda 261inayotarajia kukamilika mapema mwakani.
“Lakini pia tutakuwa na utoaji wa huduma ya kipimo cha t-scan, pia tunakamilisha ufungaji wa mashine
ya kusafisha figo, uwekaji wa mfumo wa kuzalisha hewa ya oxygen na mwaka ujao
wa fedha tunatarajia kujenga jengo jingine la kisasa kwa ajili ya wagonjwa wa nje
na dharula,” alisema Samike
Aidha kuhusu chanjo ya Covid 19 alisema Hospitali
ilipokea chanjo ya Johnson &Johnson na dozi 3050 na uchanjaji ulianza tarehe 3
Agosti, 2021 na kupitia uhamasishaji, wananchi walijitokeza na kupokea chanjo hiyo.
Sambamba na hilo aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mwanza
kujitokeza katika hizi siku tano kupata vipimo vya magonjwa mbalimbali huku
akiuomba uongozi isiwe mwisho kuweka kambi za namna hiyo.
“Tunashukuru sana uongozi wa hospitali kwa kutoa
huduma hii na niuombe uongozi hii isiwe
mwisho angalau kila baada ya muda fulani
mfanye jambo kama hili lakini pia
wananchi mjitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuja kupata vipimo vya magonjwa
mablimbali kwani madaktari hawa kuwapata uwa ni kazi sana,” alisema Samike
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya
Sekouture na Daktari Bingwa wa Watoto Dkt. Bahati Peter Msaki alisema huduma
zitakazotolewa kwa siku tano ni madaktari bingwa wa watoto, akina mama,
upasuaji na magonjwa ya ndani.
Alisema lengo la kambi hiyo ni kupeleka huduma
karibu na wananchi kwa urahisi zaidi na
kwa kupunguza gharama ambapo kumuona daktari Bingwa itakuwa ni nusu ya gharama
halisi ambazo mwananchi angetakiwa kulipia.
“Hospitali imefanya maboresho mbalimbali ikiwemo
kununua mashine za maabara za kutosha , kununuliwa kwa mashine kubwa ya mionzi,
ununuzi wa dawa za kutosha na lengo ni kutoa huduma bora kwa gharama nafuu
hivyo wananchi waje kwa wingi katika kipindi hiki kwa ajili ya kuangalia afya
zao,” alisema Dkt Bahati
Aliongeza kuwa kumuona Daktari Bingwa itakuwa ni
shilingi elfu kumi (10,000) tu ila kwa vipimo kama shinikizo la damu, uzito,
kisukari, homa ya ini, saratani ya matiti na kizazi vipimo vyake vitatolewa
bure.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata vipimo katika kambi hiyo wameushukuru uongozi wa hospitali na serikali kwa ujumla kuona haja ya kufanya hivyo kwani gharama za kuwaona madaktari bingwa huwa ni kubwa na baadhi yao hushidwa kuzimudu.
0 comments:
Post a Comment