METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 19, 2021

TWCC MWANZA WAIOMBA SERIKALI KUWAPA MAENEO YA KUJENGA JENGO LA KUZALISHA BIDHAA ZAO NA MASOKO YA KUUZIA


Emil Kasagara Katibu Tawala Msaidizi na Mkuu wa kitengo cha Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza.

Mwenyekiti wa TWCC Mkoani Mwanza Fausta Ntara

Katibu Msaidizi wa TWCC Mkoani Mwanza Jane Simon Ndeto

Shabani Mkongoti Afisa Masoko GS 1 Tanzania


Wanawake wafanyabiashara na wananchama wa TWCC.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameutaka uongozi wa chama cha wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC)  kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa na Mkuu wa kitengo cha uchumi na uzalishaji ili kuongea na  Wakurugenzi wa Halmashauri  kwa lengo la kuwatafutia maeneo ambayo watakuwa wakizalisha na kuuzia bidhaa zao.

Maagizo hayo yametolewa Oktoba 19, 2021 Jijini Mwanza na Emil Kasagara Katibu Tawala Msaidizi na Mkuu wa kitengo cha uchumi na uzalishaji cha Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel aliyekuwa mgeni rasmi wakati akizungumza na wafanyabiashara wanawake na kusema  Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa uchangiaji wa uchumi unaofanywa na wanawake kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na wao wako bega kwa bega katika kusaidia juhudi hizo.

“Nimesikia katika risala yenu mkitaja kukosekana kwa eneo la kuzalishia na kufanyia biashara kuwa ni changamoto kubwa kwenu kushindwa kufikia malengo , kimsingi Mkoa hauna maeneo, maeneo yote yapo chini ya Halmashauri hivyo namuelekeza Katibu tawala Mkoa na Mkuu wa kitengo cha uchumi na uzalishaji kukutana nanyi ili muombe kukutana na wakurugenzi wa halmashauri wawasaidie kupata hayo maeneo.” Amesema

Aidha amewataka kuandaa andiko ambalo litaelezea eneo wanalotaka, ukubwa wa eneo, shughuli watakazofanya katika eneo hilo ili iwe rahisi kwa Wakurugenzi kuwapa maeneo ambayo yataenda sambamba na mahitaji yao.

Kuhusu kukosa soko la bidhaa zao amewataka wafanyabiashara hao  kuzalisha bidhaa zenye ubora kwani ndo njia pekee za kuwashawishi watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa nchini na pia zitaleta ushindani katika soko la bidhaa.

“Mmesema bidhaa zenu hazinunuliwi na Watanzania, labda niwaambie kitu hakuna mtu ambaye atapenda kununua bidhaa ambayo haina ubora lakini mkiwa na bidhaa bora mtauza kwani kuna msemo unaosema kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza hivyo mkizingatia vitu vyote ikiwemo bidhaa kuwa na viwango, kupitishwa na mamlaka zikiwemo TBS, TMDA  kuwa na barcode nawahakikishia zitauzwa tu.” Amesema

Pia amewataka wanawake hao, kutumia chama chao kwa ajili ya kuziendea taasisi za kifedha kukopa ili kuendeshea shughuli zao pamoja na zile asilimia 4 ambazo  zinazotolewa na halmashauri zisizo na riba yoyote kwa wanawake.

“Kila Halmashauri imetenga asilimia 10 za fedha kwa ajili ya makundi ya wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2 kwa kutumia mikopo ya fedha hizi mnaweza kuongeza mitaji ya biashara zenu na mkumbuke kuwa fedha hizi hazina riba changamkieni fursa hii.” Amesema

Akizungumza wakati wa kongamano hilo mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Mwanza Bi Fausta Ntara amesema chama mpaka sasa kinawanachama 1070 pamoja na tawi moja lililopo Wilayani Magu ambalo limefunguliwa mwaka huu lakini wanamalengo ya kufungua matawi katika kila wilaya ili kuwafikia wanawake  popote pale walipo na wao wafikiwe na fursa mbalimbali.

Katika Risala yao iliyosomwa na katibu msaidizi wa chama hicho Mkoani hapa Bi Jane Simon Ndeto imesema lengo mahususi la TWCC ni kuwawezesha wanawake wajasiliamali kupambana kikamilifu katika kukuza uchumi, kuwawezesha wanawake kuona fursa mbalimbali za kibiashara na kuzitumia kwa lengo la kuwa na biashara endelevu zenye kuleta tija kwa wanawake na kuwajengea uwezo wa kujiamini katika kusimamia biashara zao.

Ameyataja mafanikio waliyoyapata ikiwemo kuongezeka kwa wanachama pamoja na changamoto zikiwemo ukosefu wa maeneo ya kuzalishia na kuuzia bidhaa, masharti upatikanaji wa vibali vya kuzalisha bidhaa kutoka TBS, TMDA, BARCORD, OSHA  kodi na tozo kuzidi, mitaji midogo, masharti magumu ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha pamoja na watanzania kutopenda bidhaa zinazozalishwa nchini.

Aidha wameiomba serikali kupunguza masharti ya upatikanaji wa bidhaa,  kupunguzwa kwa kodi na tozo zipunguzwe pamoja na kupatiwa eneo ambalo watajenga jengo la kuzalisha bidhaa na masoko ya kuuzia bidhaa pamoja na kuomba fedha za mradi wa vifungashio kwa ajili ya wajasiliamali wote Mkoani Mwanza na Mikoa ya jirani. 

Kupitia kongamano hilo wanawake hao walipewa elimu juu ya faida mbalimbali za kuwa na barcode kwenye bidhaa zao kutoka GS1 Tanzania ambapo kupitia afisa masoko wao Shabani Mkongoti amesema mbali na kuongeza thamani ya bidhaa barcode pia hutambulisha bidhaa kimataifa na kupata mrejesho wa bidhaa sokoni pamoja na kuongeza wigo wa biashara.

Amesema barcode humuwezesha mfanyabiashara kufahamu kifungashio gani huwezesha bidhaa kuuzwa Zaidi sokoni, hulaisiha mfumo wa mauzo na hutumiwa dunia nzima ,huleta  faida kwa nchi, kwa wajasiliamali na muuzaji wa rejareja na kwa nchi zinazoendelea wanunuzi hutumia barcode kuitambua bidhaa ilivyotengenezwa mpaka gharama yake.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com