Na: Projestus Binamungu, WHUSN-Kahama
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi
zenye uhuru wa vyombo vya habari akisisitiza uhuru huo kuenda sambamba na
wajibu.
Waziri Bashungwa ametoa kauli
hiyo Septemba 3 2021, wakati akizindua kituo cha matangazo mjini Kahama mkoani
Shinyanga kilichopewa jina la Gold Fm ikiwa na kauli mbiu ya Sauti ya dhahabu.
Akizungumza katika mahojiano
maalum mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho
Waziri Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Rais
Samia Suluhu Hasaan inathamini na kuamini katika uhuru wa vyombo vya habari
kupaza sauti za watanzania ili kuyafikia matamanio yao.
Waziri Bashungwa amekaririwa
akisema “Serikali ya awamu ya sita kwa kuthamini uhuru wa vyombo vya habari
inakusudia kuondoa asilimia 50 ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye
marekebisho ya kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika
redio na televisheni”
Ameongeza kuwa “Wamiliki wa
mitandao ya kijamii kama YouTube ambayo maudhui yake siyo ya kihabari
wataruhusiwa kupakia video zao mitandaoni bure, kama sehemu ya kuwawezesha
kujitangaza na kujiingizia kipato zaidi”.
“Ninafurahi kuona uwekezaji
wa namna hii unaenda sehemu husika(Kahama), suala la kuanzisha television
nawashauri mkiweza anzeni mapema na mkihitaji msaada tuambieni hiyo ndiyo kazi
yetu” Alisema Waziri Bashungwa.
Katika hatua nyingine Waziri
Bashungwa amezungumzia maendeleo ya mchakato wa kupata vazi la taifa amesema Serikali kupitia wizara yake
inakusudia kuwakutanisha wabunifu wa mavazi wa hapa nchini na kuwapa fursa ya
kubuni vazi litakalo shindanishwa na kupigiwa kura ili kupata mavazi kadhaa
yatakayotumika kama mavazi rasimi ya kumtambulisha mtanzania.
“Serikali iliona ni vyema
iandae utaratibu ambao kupitia kwa wabunifu wa mavazi wenye wabuni na waseme
kuwa hili linafaa kuwa vazi la taifa, na vazi hili siyo lazima liwe moja,
yanaweza kuwa hata mawili n ahata matatu lakini yale ambayo yatashindanishwa na
kushinda” alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza katika uzinduzi
huo Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis
Mihayo amewataka watangazaji na waandishi wa habari kuwa wabunifu zaidi ili
kuitendea haki leseni ya utangazaji inayotolewa na mamlka hiyo kwa nia ya
kuwawezesha watanzania kuhabarishwa kwa ubunifu zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
kituo cha Gold FM Bi Neema Mghen ameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo kupitia Baraza la Sanaa Tanzania BASATA kwa kushirikiana na Wizara ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
TCRA kuvijengea mazingira wezeshi vituo vichanga vya redio ili viendelee kuwa
daraja la kuwasaidia wasanii wachanga kutimiza ndoto zao.
Uzinduzi wa kituo hicho cha
redio cha Gold FM kinaifanya wilaya ya Kahama kuwa na vituo Vinne vya redio
huku kwa mkoa wa Shinyanga vikifika vituo vitano ambavyo ni redio Gold FM,
Kahama FM, Divine FM, Huheso FM na Radio Faraja Fm.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment