METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 15, 2021

UFUNGAJI WA MKUTANO WA MAKATIBU TAWALA MAKAMANDA POLISI MIKOA NA WADAU KUHUSU MIKAKATI YA KUONDOKANA NA WATOTO WANAOISHI MITAANI


Na Mwandishi wetu Dodoma

 

Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa kutokomeza watoto wanaoishi mitaani wameazimia kuanza ukaguzi wa magari ya abiria ili kubaini usafirishaji wa watoto kwa lengo la kuzuia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

 

Hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja cha Makatibu Tawala wa Mikoa, Makamanda wa Polisi na Wadau wanaoshughulika na kutokomeza watoto wanaoishi mitaani, kilichofanyika Jijini Dodoma.

 

Katika kikao hicho, wamekubaliana kuwa Jeshi la Polisi lianze kutambua watoto wote wanaoishi na kufanya kazi mitaani ili kuwarejesha kwenye familia zao na kuiomba Wakala wa usafirishaji LATRA na Wadau wa usafiri kuweka mfumo madhubuti wa usafirishaji watoto.

 

Wamesema ukaguzi wa vyombo vya usafiri hautahusisha ubovu tu wa magari bali hadi kwenye Chesesi ili kubaini usafirishaji wa watoto,ikiwezekana kuwekwa utaratibu wa kuandika umri wa wasafiri.

 

Aidha, Wadau hao wamesisitiza Jamii kuhamasishwa zaidi kuhusu malezi, matunzo na ulinzi ya watoto kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo vyombo vya Habari na nyumba za Ibada.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu Kamanda Benedict Wakulyamba ameishukuru Wizara kwa kuwashirikisha wakiwa ni Wadau muhimu katika kumaliza changamoto hiyo kwani Jeshi la Polisi linahusika moja kwa moja na makundi yanayoshughulikiwa na Wizara na  jukumu lao ni kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kutokomeza tatizo hili.

 

Akihitimisha kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Jingu, amesema kuna kila sababu ya kuwalea watoto vizuri ili kuondokana na changamoto hiyo na kuwahamasisha Wadau wote kuweka nia thabiti ya kupambana na tatizo hilo kikamilifu.

 

"Tumefikia Maazimio ya jumla ya kila Taasisi na kama yatatekelezwa ipasavyo uwezekano wa kuondokana na changamoto hii ya Watoto waishio katika Mazingira hatarishi ni mkubwa” alisisitiza Dkt Jingu.

 

Akiwasilisha mada kuhusu haki ya mtoto, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Lucy Saleko alisema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inawataka wazazi kuwajibika kuwalinda watoto wao dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa aina yoyote vinginevyo watachukuliwa hatua.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com