METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 31, 2018

KAYA MASIKINI 3912 KUNUFAIKA NA TASAF MZUNGUKO 16 ILEMELA

Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imehawilisha jumla ya shilingi Milioni 143,704,00.00 kwa kaya 3912 kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF)

Akizungumza katika zoezi la uhawilishaji wa fedha hizo mratibu wa TASAF manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh amesema kuwa hii ni awamu ya tatu tangu kuanza kwa mpango huo ikiwa na mzunguko wa kumi na sita utakaojumuisha wanufaika wa mitaa yote ya kata kumi na nane za Kayenze, Sangabuye, Bugogwa, Shibula, Buswelu, Kiseke, Kirumba, Nyamhongolo, Nyakato, Nyasaka, Kawekamo, Pasiansi, Mecco, Buzuruga, Ilemela, Kitangiri na Nyamanoro zilizopo kwenye mpango ikiachwa kata moja ya Kahama ambayo haipo kwenye mpango huo

'.. Tunategemea kuzifikia kaya 3912 zinazonufaika na mpango huu wa kunusuru kaya masikini katika mzunguko huu wa kumi na sita ambapo zaidi ya milioni mia moja na arobaini na tatu tutazihawilisha kwa walengwa kusudiwa ..' Alisema

Kwa upande wake afisa ufuatiliaji wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kwa mkoa wa Mwanza Ndugu Kagwe Samson Kagwe amewaasa wananchi wanaonufaika na mpango huo kuhakikisha wanazitumia vizuri fedha hizo kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji itakayowakwamua kutoka katika umasikini huku akionya serikali itawachukulia hatua watu wasio waadirifu wanaokwamisha zoezi hilo pamoja na walengwa watakaotumia vibaya fedha hizo ikiwemo unywaji wa pombe

Akihitimisha mwenyekiti wa mtaa wa Bugogwa ndugu  Kongwe Aloyce Kongwe mbali na kuishukuru Serikali kwa kuendelea na mpango huo uliosaidia wananchi wake kuweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kupeleka watoto shule, kuanzisha miradi midogo midogo ya bustani za mboga mboga na biashara ameiomba kuona namna bora itakayo wafanya watu wenye sifa ambao walipuuza kujiunga na mpango wa kunusuru kaya masikini  wakati wa zoezi la  kuhakiki wanufaika ili waweze kurudishwa kwenye mpango na kunufaika

Zoezi la uhawilishwaji wa ruzuku hiyo kwa kaya masikini ulihusisha pia ukaguzi wa miradi inayofanywa na baadhi ya kaya za mfano zinazonufaika na mradi huo

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com