METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 14, 2020

NAIBU WAZIRI WA NISHATI ATAKA WANANCHI WAHAMASISHWE KUTUMIA UMEME

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Mazae kilichopo katika kata ya Mazae, Wilaya ya Mpwapwa,Mkoani Dodoma, Agosti 13,2020.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiongea na wananchi wa Kijiji cha Maza , kata ya Mazae, Wilaya ya Mpwapwa,Mkoani Dodoma, wakati akiwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa usambazaji umeme vijijini Agosti 13,2020.

Wananchi wa Kijiji cha Mazae  kata ya Mazae, Wilaya ya Mpwapwa,Mkoani Dodoma, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu(hayupo pichani) wakati akiwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa usambazaji umeme vijijini Agosti 13,2020.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka viongozi wa Serikali za mitaa kuwahamasisha wananchi wanaoishi katika  maeneo yao kutumia huduma ya umeme kwa kulipia huduma hiyo  ili waweze kuunganishwa na huduma hiyo.

Ameyasema hayo, Agosti 13, 2020 wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi ya kazi ya usambazaji umeme vijijini katika kijiji cha Mazae, kata ya Mazae,Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma kabla ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi ya Mazae kijijini humo.

Alisema kuwa,hajaridhishwa na kasi ya uunganishwaji wa umeme katika kijiji hicho na kuwataka viongozi mbalimbali  wa vijijini kufanya mikutano ya kuwamasisha wananchi wa maeneo yao kulipia huduma ya umeme  ili wananchi wafaidike na huduma hiyo ambapo Serikali inatumia gharama kubwa kufanikisha jambo hilo.

Naibu Waziri, ameyataja baadhi ya maeneo ambayo huduma ya umeme imefika lakini wananchi wa maeneo hayo bado hawajalipia huduma hiyo, maeneo hayo ni pamoja na Isomvu,Chungu,Darajani, Nyabu na maeneo mengine katika kijiji hicho.

“Serikali imepunguza gharama ya kuunganisha umeme vijijini ambayo ni 27,000 tu huu mradi unakaribia kufika ukingoni wananchi wanaonekana hawajalipia na Mkandarasi amesema kuwa wananchi wakilipa yeye yupo tayari kuwaunganishia kwahiyo niwaombe wananchi wapo kwenye wigo maeneo ambayo mradi umefika mlipie ili mpata kunganishiwa umeme,”alisema. 

Amewaeleza wananchi wa kijiji hicho kuwa, Serikali  inafanya kazi kubwa kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya umeme na tayari imeingia katika utekelezaji REA III mzunguko wa pili na mradi mwengine wa ujazilizi ambapo Mkoa wa Dodoma upo kwenye miradi hiyo na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili iwasaidia katika kujiendeleza kimaendeleo katika maeneo yao. 

Aidha, amesema kazi ya usambazaji umeme nchini inapimwa kwa wananchi wengi kupata huduma hiyo ili wateja wengi wapatikane na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lijiongeze wateja na mapato na liweze kujiendesha wenyewe.

Ameongeza kuwa,miradi mingi nchini inatekelezwa bila ya elimu ya kutosha kwa wananchi ambapo wananchi wengi hawapati elimu ya kutosha kuhusu miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa wananchi hao katika kujikwamua kiuchumi.

Pia, aliwaeleza wananchi wa kijiji kuwa zaidi ya bilioni 800 zimetengwa kwaajili ya kazi ya usambazaji umeme ambapo kuanzia tarehe 20 mwezi huu mpaka Septemba mwaka huu Serikali itakuwa inakabidhi kazi ya usambazaji umeme kwenye vijiji na vitongoji nchini kwa wakandarasi wapya.

Aidha, amewataka wananchi ambao vijiji na vitongoji vyao bado havijafikiwa na miradi ya umeme kutokuwa na hofu kwababu miradi inayokuja maeneo yao yatafikiwa na miradi hiyo na kuwaeleza kuwa tayari Serikali imeshapeleka umeme kwenye vijiji takribani 9512.

Naye, Hamis Israel ambae ni mwanakijiji wa kijiji hicho ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya umeme katika kijiji chao na kuitaka Serikali kuondoa changamoto wanazozipata wananchi wakati akiwa wanahitaji huduma hiyo.

Katika ziara yake hiyo Naibu Waziri wa nishati pia alikagua kazi ya usambazaji umeme Mkoani Morogoro katika wilaya ya Kilosa na kuwashaa umeme katika kijiji cha lumuma kilichopo katika kata ya Lumuma na baadae kugagua umeme katika nyumba na maeneo ya biashara ambayo tayari wamewapelekewa umeme.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com