METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 27, 2021

TANZANIA MWENYEJI WA MSHINDANO YA UREMBO, UTANASHATI NA MITINDO KWA VIZIWI AFRIKA

Mlimbwende atakayeiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Watu Wenye Usikivu Hafifu (Viziwi)  Afrika yatakayofanyika Oktoba 01, 2021 Jijini Dar es Salaam.    Baadhi ya wageni waliowasili Tanzania tayari kwa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Watu Wenye Usikivu Hafifu (Viziwi)  Afrika yatakayofanyika Oktoba 01, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Na Eleuteri Mangi, WSUM, Dar es Salaam

Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Watu Wenye Usikivu Hafifu (Viziwi) Bara la Afrika yatakayofanyika Oktoba 01, 2021 katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yanaandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Kituo cha Sanaa Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) pamoja na nchi washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika  ambayo yatawahusisha vijana wa kike na wa kiume ambao wengi wao tayari wamewasili jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuanza kambi ya maandalizi kuelekea mashindano hayo kuanzia Septemba 26 hadi 30, 2021.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema kutokana na umaalumu wa kundi hilo, kimkakati italitangaza Taifa hili kimataifa, ambapo Tanzania inaendelea kujipambanua kama nchi inayojali na kuthamini watu wote bila kujali changamoto zao za kimaumbile.

“Tanzania kwa sasa ipo katika kipindi maalumu cha kujitangaza kimataifa kupitia programu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ijulikanayo kama “Rebranding Tanzania. Kuoitia umaalum wa kundi hili, na kupitia fursa ya mashindano haya, Tanzania inapata nafasi ya kuuonesha ulimwengu namna inavyojali na kuthamini watu wote bila kujali changamoto zao za kimaumbile”, amesema Dkt. Ishengoma.

Katika kuhakikisha washiriki wa Tanzania wanaliwakilisha vema Taifa letu, Serikali kupitia Wizara hii imewawezesha washiriki wake nane ambao watashiriki mashindano hayo ambapo kila mshiriki amewezeshwa kifedha kupata maleba na mahitaji mengine kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mshiriki.

Vile vile, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na sekta ya Sanaa imegharimia  malazi, chakula, usafiri wakati wote wa mashindano kutoka na kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere Dar es salaam pamoja na maeneo yote watakayotembelea washiriki hao ikiwemo fukwe za bahari ya Hindi na maeneo mengine wakati wote wa maandalizi hadi mwisho wa mashindano hayo ambayo kilele chake ni usiku wa Oktoba 01, 2021.

“Kipaji ni zawadi ya Mungu kwa watu wote ili waweze kumudu maisha yao na karama hii hutolewa bila kujali changamoto za kimaumbile wanazoweza kuwa nazo wahusika. Hivyo, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya kutambua na kukuza vipaji hivyo inao wajibu wa kutekeleza jukumu hilo kwa kushirikisha watu wote bila kuangalia changamoto zozote za kimaumbile”.

Aidha, Dkt. Ishengoma ametoa wito kwa watu wote  wanaothamini mchango wa Sanaa katika kuzalisha ajira na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja, wajitokeze kwa wingi kudhamini mashindano hayo na kuhudhuria kwa wingi kuwashuhudia vijana wanavyoonesha vipaji vyao katika ukumbi wa hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.  

Jumla ya washiriki 85 kutoka nchi 30 barani hapa wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo ambapo hadi sasa Septemba 27, 2021 jumla ya washiriki 37 tayari wamewasili nchini kutoka mataifa ya Burundi, Botswana, Uganda, Kenya, Senegal, Rwanda na wenyeji Tanzania tayari kwa maandalizi kuelekea mashindano hayo.

Tanzania inawakilishwa na Mlimbwende Khadija Kanyama ambaye alitwaa taji hilo katika mashindano yaliyofanyika nchini Agosti 14, 2021 jijini Dar es salaam katika ngazi ya Taifa na kwa upande wa wanaume atakayewakilisha taifa ni mtanashati Rajani Ally wakati kwa upande wa mitindo mwakilishi ni Carloyne Mwasaka kwa wananwake na kwa upande wa wanaume mwakilishi atakuwa Russo Songoro .

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com