Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (katikati), akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Shigunga, Eneo la Mandu Makaburini, wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, Ezekiel Shiula (kulia), wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 6, 2021. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kishiri wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, Amos Shilangi (kulia) akielezea hali ya upatikanaji wa umeme katika eneo hilo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto), wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 6, 2021. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Oswald Urassa (kulia) akiteta jambo na Meneja Mradi wa Kampuni ya Ukandarasi ya Segemcom, Mhandisi Adrian Mapunda wakati wa ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Mwanza, Septemba 6, 2021.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo akimtambulisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga (kushoto) kwa watoto wakazi wa Mtaa wa Kishiri wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, Septemba 6, 2021. Bodi ilikuwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Kazi ya kusambaza umeme vijijini ikiendelea katika Kitongoji cha Mwahuli, Kata ya Isangijo Kisesa, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 6, 2021.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kulia) akizungumza na Mkazi wa Kitongoji cha Mwahuli, Kata ya Isangijo Kisesa, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, John Masalu wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 6, 2021. Wa pili-kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Kikao baina ya Bodi ya Nishati Vijijini, Watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mwanza, Septemba 6, 2021. Bodi ilikuwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto – mwenye kofia), akitoa maelekezo kwa Watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mwanza, kutatua changamoto ya mkazi wa Kitongoji cha Mwahuli Kisesa, wilayani Nyamagana, mkoani humo, Magret Komanya (kushoto kwa Mwenyekiti), ambaye nyumba yake ilirukwa wakati wa kuunganisha umeme wakazi wa eneo hilo. Bodi ilikuwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 6, 2021.
Veronica Simba – Mwanza
Wananchi mbalimbali mkoani Mwanza wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Pongezi hizo zilitolewa na viongozi wa vijiji mbalimbali mkoani humo wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, Septemba 6 mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Wakili Julius Kalolo, ambaye alifuatana na mmojawapo wa Wajumbe wa Bodi Oswald Urassa, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Amos Maganga pamoja na Wataalam mbalimbali kutoka REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), viongozi hao walikiri wananchi kunufaishwa na miradi husika.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Shigunga wilayani Nyamagana, Ezekiel Shiula alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa eneo lake kufikiwa na umeme wa REA ambao umewasaidia pamoja na mambo mengine kuondoa tatizo sugu la vibaka lililokuwa likiwasumbua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bushitu, Eneo la Kishiri, wilayani Nyamagana, Amos Shilangi alieleza kuwa, wananchi katika eneo lake wamehamasika na kuchangamkia fursa ya umeme wa REA kutokana na gharama ya kuunganishwa kuwa nafuu yaani shilingi elfu 27 tu.
Aidha, John Masalu ambaye ni mwananchi wa Kitongoji cha Mwahuli, Kijiji cha Isangijo, Eneo la Kisesa wilayani Magu, aliipongeza Serikali kwa kuwapunguzia ukali wa maisha wakazi wa eneo hilo kwa kuwapelekea mradi wa REA, ambapo umewawezesha kuanzisha biashara ndogondogo zinazowaingizia kipato.
Katika hatua nyingine, Wakili Kalolo aliwaelekeza watendaji wa REA na TANESCO kutafuta namna ya kutatua changamoto ya Mkazi wa Kitongoji cha Mwahuli, Magret Komanya ambaye nyumba yake imerukwa kutokana na eneo ilipo kuwa pembeni mbali na njia ya umeme. Aliwaagiza kuhakikisha Mama huyo anapata umeme.
Akizungumza na viongozi na wananchi wa maeneo mbalimbali wakati wa ziara hiyo, Wakili Kalolo aliwataka wawe Mabalozi wa kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa ya umeme wa REA kwa kuhakikisha wanaandaa mazingira wezeshi ya nyumba zao kuunganishiwa umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Maganga aliwasihi wananchi ambao wamerukwa ilhali umeme ulikwishafika katika maeneo yao kuwa na subira, akifafanua kwamba Mradi wa Ujazilizi unaoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali umelenga kuwafikia wote kwa kujaziliza pale palipoachwa kutokana na sababu mbalimbali.
Bodi ya Nishati Vijijini iko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika mikoa mbalimbali nchini.
0 comments:
Post a Comment