Waziri wa Kilimo, Prof Adolf
Mkenda akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa
Ushirika yaliyofanyika katika ukumbi wa BOT mkoani Mtwara, jana. (Picha Zote Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo, Prof Adolf
Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Hussein Bashe wakiwa wameongozana na viongozi
wengine wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakikagua maghala yaliyopo
katika bandari ya Mtwara kuelekea kuanza msimu wa uuzwaji wa korosho ambao
unatarajiwa kuanza hivi karibuni wakati wa ziara ya Waziri Mkenda bandarini
hapo, Tarehe 20 Septemba 2021.
Waziri wa Kilimo, Prof Adolf
Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Hussein Bashe wakiwa wameongozana na viongozi
wengine wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakikagua utayari wa bandari
ya Mtwara kuelekea kuanza msimu wa uuzwaji wa korosho ambao unatarajiwa kuanza
hivi karibuni wakati wa ziara ya Waziri Mkenda bandarini hapo, tarehe 20 Septemba 2021.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Prof Adolf
Mkenda amesema Bandari ya Mtwara imejiandaa vizuri kwa ajili ya kusafirisha zao
la korosho na uamuzi huo hautabadilika kwa kuwa ni maekezo ya Rais Samia Suluhu
Hassan.
Aidha, amepiga marufuku
matumizi ya kangomba kwenye mauzo ya zao hilo huku akieleza kufanya hivyo
kutachelewesha kuuzwa kwa bei nzuri na watu kuandaa mashamba kwa wakati.
Hayo ameyasema mjini Mtwara wakati
alipotembelea bandari hiyo kwa lengo la kuangalia kama maelekezo ya Rais kuhusu
korosho yote kusafirishwa kupitia hapo yametekelezwa.
“Haya ni maelekezo ya
serikali kwamba korosho yote huku itapitia bandari hii maagizo hayo ni ya Rais
hayatabadilika kwa hiyo wote ambao wanataka kufanya biashara ya Korosho
wajipange “
“Zaidi ya hapo hapa bandarini
wanafanya kazi saa 24 kwa hiyo meli
ikija kama ni kupakia inapakia kwa muda na kasi sana kwa sababu ya uwezo huo wa
kufanya kazi muda wote,” amesema.
Amesema kuwa Serikali
imeshatoa kibali wanaosafirisha korosho kuleta bandari ya Mtwara wanaruhusiwa
kufanya hivyo kwa saa 24 hivyo wameshatengua kanuni zilizokuwa zinaeleza baada
ya saa 12 huwezi kusafirisha zao hilo.
Amesisitiza kuwa mtu akitaka
kununua korosho lazima apitishe kwenye Bandari hiyo kwakuwa gharama
zimepunguzwa hivyo kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kusafirisha kwa njia
nyingine.
“Tunasisitiza si kwa sababu
tunataka bandari hii ifanye kazi bali uzoefu unaonyesha kwamba korosho
inaponunuliwa kutoka Mtwara yenye ubora inaposafirishwa mpaka Dar es Salaam
baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiiharibu kwa
kuongeza vitu au kuweka isiyofaa.
Katika hatua nyingine amepiga
marufuku matumizi ya kangomba huku akieleza kwa kufanya hivyo kutachelewesha
kuuza kwa bei nzuri bidhaa hiyo na watu kuandaa mashamba kwa wakati.
Naibu Waziri wa kilimo,
Hussein Bashe amesema wataendelea kufanya kazi na mamlaka ya Bandari na kupitia
kikao kitakachofanyika Alhamisi jijini Dar es Salaam watajadili hoja mbalimbali
zilizotolewa na wasafirishaji wa zao hilo.
Amezitaja baadhi ya hoja hizo
ni gharama ya uhifadhi, upatikanaji wa makasha, muda wa kuhifadhi makasha ya
wasafirishaji ambao kwa sasa umeongezwa kutoka siku 14 mpaka 21, uwezo uliopo
ni kuhifadhi makasha 13000 kwa wakati mmoja hivyo hakuna tatizo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Karim Mattaka amesema wapo tayari kuhudumia
shehena hiyo kwa kuwa wameongeza uwezo
wa kuhifadhi na kuhudumia korosho kwa kuongeza eneo na vifaa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment