Na Teresia Mhagama, Songwe
Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani, amesema kuwa tathmini ya agizo la Serikali la kupeleka umeme
mijini na vijijini kwa shilingi 27,000 itafanyika ndani ya miezi mitatu ili
kuona kama agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.
Waziri wa Nishati alisema
hayo tarehe 27 Agosti, 2021 wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe wakati akizungumza
na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Cosmas Ishenye, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna
Gidarya na Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole
kabla ya kuzindua kimkoa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya
Tatu, Mzunguko wa Pili.
“ Suala la kupelekewa umeme
kwa zaidi ya shilingi 27,000 halipo, pia suala la mwananchi kuuziwa nguzo halipo,
mtu awe tajiri au maskini bei ni moja tu ambayo ni shilingi 27,000 tu hivyo
tutafuatilia kuona kama agizo hili linafanyiwa kazi na watendaji wetu.” Alisema
Dkt. Kalemani
Alisema Serikali inataka
wananchi wengi waunganishiwe umeme ili wautumie kwa shughuli mbalimbali hivyo
aliwaagiza watendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya
kusambaza umeme na kuacha kuweka vikwazo vya kumpelekea mwananchi umeme kama
vile malipo ya nguzo.
Akizungumzia hali ya
upatikanaji umeme kwa Mkoa wa Songwe alisema kuwa, kwa sasa Mkoa huo umejengewa
kituo kidogo cha kupoza umeme wakati Serikali ikifanya jitihada nyingine za
kupeleka umeme wa uhakika mkoani humo.
Aliongeza kuwa, kuna mradi
mkubwa wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Iringa, kupitia Mbeya, Tunduma
hadi Sumbawanga ambao utaimarisha zaidi hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa
hiyo pamoja na Songwe ambapo mkandarasi anatarajiwa kuanza kazi mwezi Februari
mwakani.
Akiwa wilayani Mbozi, Waziri
wa Nishati alikagua kituo kidogo cha kupoza umeme wilayani humo na kuiagiza
TANESCO kuanza kupeleka umeme kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo ndani ya siku
Kumi baada ya wananchi hao kulalamika
kuwa hawana umeme.
Awali, Meneja wa TANESCO Mkoa
wa Songwe, Grace Mtungi alisema kuwa mahitaji
ya juu ya umeme mkoani humo ni megawati 13.5 huku uwezo wa mitambo ya umeme
ukiwa ni megawati 15 hivyo Mkoa huo
unapata umeme wa kutosha mahitaji kwa sasa.
Aliongeza kuwa, idadi wa
wateja waliounganishwa na umeme inaendelea kuongezeka kwani katika mwaka
2019/2020 wateja waliounganishwa umeme walikuwa ni 51,176 na kwa sasa kuna
wateja 58,587.
Katika hatua nyingine, Waziri
wa Nishati alizindua Mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu,
Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Songwe ambao unatarajiwa kusambaza umeme katika
Vijiji 127 kwa gharama ya shilingi bilioni 42.3.
Katika uzinduzi huo, Waziri
wa Nishati aliitaka kampuni ya Derm Electrics kufanya kazi ya usambazaji umeme
mkoani humo kwa muda wa miezi 18 kwa kutumia vifaa vinavyopatikana nchini.
Kuhusu hali ya usambazaji umeme vijijini nchini, alisema kuwa, mpaka sasa takriban vijiji 10,312 vimeshasambaziwa umeme na vimebaki vijiji 1956 huku lengo likiwa ni Vijiji vyote kuwa na umeme ifikapo Disemba mwakani.
0 comments:
Post a Comment