METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, July 10, 2021

HAIJAWAHI KUTOKEA, KATIBU MWENEZI TAIFA SHAKA ALALA NYUMBANI KWA BALOZI NA KUPATA CHAI NA UONGOZI WA SHINA HILO

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndugu Shaka Hamdu Shaka amelala nyumbani kwa Balozi  Ndugu Iddi Mwaibaje  mwenyekiti wa shina namba 1 Kata ya Chapwa Jimbo la Tunduma. Asubuhi ya leo amejumuika na uongozi na wanachama wa shina hilo kupata chai pamoja.

Akiwa katika shina hilo Ndugu Shaka aliushukuru uongozi na wanachama wa shina kwa ukarimu na kuwataka viongozi wengine wa chama na serikali kuwa na utamaduni wa kupenda kukaa na kula pamoja na wenyeviti wa mashina kwani inawapa ari zaidi katika majukumu yao na kujenga mshikamano kati yao. Pia aliwasilisha salaam za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo kwa wanachama wa shina hilo.

Alieleza madhumuni ya ziara yao ni kuendelea kuimarisha uhai wa Chama na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025. Aidha pamoja na madhumuni hayo wanasikiliza na kupokea kero za wananchi kwa ajili ya kusukuma utatuzi wake.

Amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa halmashauri ya mji Tunduma kwa kuiamini CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwachagua madiwani wote, Mbunge na Rais kwa ushindi wa kishindo.

"Imani yenu kwa CCM tutailinda, tutaitunza na tutaipa thamani kwa kuwaletea maendeleo ya kweli na kuimarisha huduma kwenu. Endeleeni kutuunga mkono na kumuunga mkono Mhe Rais Samia na serikali anayoiongoza." Alisema Shaka.

Alimpongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Tunduma, madiwani na wataalam wake kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ambapo aliwasisitiza ongezeko la makusanyo likaonekane kwa wananchi kwa kuimarisha huduma na kuwajengea mazingira mazuri ya kiuchumi ili washiriki vizuri katika kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com