Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeielekeza Mamlaka
ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo
imeshaingia nchini (Export Permit) badala
ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof
Adolf Mkenda ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Muwakilishi wa
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea (YARA) Ofisini kwake Jijini Dodoma
Ili kuongeza ufanisi zaidi wa
utendaji Waziri Mkenda amesema kuwa vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao
(Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa
taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.
Waziri Mkenda amesema kuwa
serikali ina matumaini makubwa na wafanyabiashara wa mbolea kwani inaamini kuwa
kurahisishwa utolewaji wa vibali hivyo kutawaongezea kasi ya kuagiza mbolea
nyingi itakayoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa ndani na nje ya
nchi.
Amesema kuwa kufuatia
uingizwaji mwingi wa mbolea nchini jambo hilo litaimarisha uwezekano wa upatikanaji
wa mbolea kwa bei nafuu kwa wakulima jambo litakalopelekea kuongezeka tija na
uzalishaji kwa wakulima.
Kuhusu gharama za
usafirishaji wa mbolea kupitia barabara, Waziri Mkenda amesema kuwa atafanya
mazungumzo na Hazina ili kuona uwezekano wa huduma za kusafirisha mbolea kama
itawezekana kutoa VAT.
“Tumegundua kuwa kusafirisha
mbolea kwa reli kunapunguza sana gharama kwahiyo tumehimiza mbolea isafirishwe
kwa reli kwenda kaskazini kwa maana ya mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na
Manyara pamoja na kusafirishwa kwa reli kupitia njia ya kati mikoa ya Morogoro,
Singida, Dodoma, Singida N.k na Tazara tutafanya hivyo” Amekaririwa Prof Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa
ili kupunguza gharama za mbolea nchini serikali imeielekeza Mamlaka ya Mbolea
TFRA kuhakikisha kuwa inaongeza muda wa zabuni ambao walikuwa wameutoa.
Kuhusu Kampuni ya Mbolea
Tanzania (TFC), Waziri Mkenda amesema kuwa katika makubaliano ya kikao kazi cha
wizara atatafutwa mtaalamu elekezi kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es salaam shule ya Biashara kukaa kwa kipindi cha miezi sita
na kuishauri serikali nini kifanyike ili kuifufua taasisi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Mazao Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu amesema kuwa Waziri wa Kilimo
ameendelea kukutana na wadau wa mbolea nchini ili kuhakishisha kuwa wakulima
wanaendelea kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara hivyo ili kufikia
hatua hiyo ni lazima kuongeza matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.
Amesema kuwa nchi mbalimbali
duniani zinaitegemea bandari ya Dar es salam katika kusafirisha mbolea hivyo
vibali vya usafirishaji wa mbolea kutolewa moja kwa moja na TFRA itaongeza
chachu ya urahisishaji kwa wauzaji wa mbolea lakini pia kurahisisha upatikanaji
wa mbolea kwa haraka.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment