Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Lindi
Kiwango cha uzalishaji na tija kwenye mazao mengi hapa nchini bado kipo chini. Kwa mfano, uzalishaji wa korosho kwa sasa ni wastani wa kilo 5 hadi 10 kwa mti ikilinganishwa na tija ya juu ya kilo 35 kwa mti inayoweza kufikiwa kulingana na viwango vya kitaalam.
Baadhi ya sababu zinazosababisha kuwepo kwa tija
ndogo kwenye mazao ni pamoja na Matumizi madogo na yasiyokuwa sahihi ya
pembejeo, Uwekezaji mdogo kwenye tafiti za kimaendeleo, Huduma duni za ugani, na Kuyumba
kwa masoko ya mazao kwenye baadhi ya misimu.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda
amebainisha hayo leo tarehe 6 Juni 2021 wakati akizungumza kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi kwenye Mkutano maalumu wa wadau wa Tasnia ya Korosho unaofanyika
katika hotel ya Sea View Resort Mkoani Lindi.
Amesema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana
na wadau imeendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya
kimkakati ikiwemo korosho ili kuongeza kipato cha mkulima na taifa kwa ujumla.
Katika zao la korosho, Waziri Mkenda amesema
kuwa jitihada hizo ni pamoja na elimu ya kilimo bora cha korosho kwa wakulima,
uzalishaji wa miche bora ya korosho, matumizi ya pembejeo, kuimarisha shuguli
za utafiti na usambazaji wa mabomba ya kupulizia viuatilifu, ambapo Vyama Vikuu
vya Ushirika vinasambaza mabomba kwenye AMCOS zote 623 nchini.
“Hadi sasa mabomba 135 yameshasambazwa kwenye
AMCOS. Mfano Mkoa wa Mtwara wenye wastani wa miche 23,918,206 ulizalishaji
ukiongezeka kufikia tija ya kilo 35 kwa mti kwa mwaka mapato ya wakulima
yataongezeka kutoka billion 279.8 za sasa hadi kufikia trilioni 1.971 kwa mwaka”
Amekaririwa Prof Mkenda
Amesisitiza kuwa ili kuendelea na juhudi za
kutatua changamoto za mazao nchini, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi
ya Korosho ilifanya kikao cha wadau wa korosho
tarehe 23 Aprili, 2021 jijini Dodoma kujadili changamoto za zao hili hapa nchini.
Katika kikao hicho, wadau walipata fursa ya
kupokea mawasilisho kutoka kwa wataalam yaliyoelezea hali ya tasnia ya korosho
hapa nchini na namna ya kuongeza tija na uzalishaji.
Miongoni mwa mawasilisho hayo ni utafiti wa
hali ya uzalishaji wa korosho uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo
Naliendele ambao ulionesha mwenendo wa kushuka kwa uzalishaji wa korosho
kutokana na matumizi madogo ya pembejeo na mabadiliko ya tabianchi.
AMesema kuwa ipo haja kama nchi kuwa na mpango
wa uhakika wa ugharamiaji wa pembejeo za zao la korosho pamoja na kuendelea
kufanya utafiti ili kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment