Said Said Nguya, CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi CCM, Ndg. Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi
wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke.
Mazungumzo hayo
yamefanyika leo tarehe 31 Mei, 2021 katika ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini
Dodoma, ambapo Balozi huyo anayemaliza muda wake nchini Tanzania ametumia fursa
hiyo kuwaaga wanaCCM na watanzania kwa ujumla, ambapo ameeleza kuwa, China na
Mataifa mengine yanafurahishwa sana na mwenendo mzuri wa uongozi wa awamu ya
sita chini ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Samia Suluhu Hassan na wanatarajia
Tanzania kuendelea kupiga hatua zaidi za maendeleo.
"Tunafuraha kuona
kwamba, uongozi mpya ndani ya Chama na Serikali chini ya Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan unaendelea vema na uongozi umendelea kuwa imara na wenye
tija kwa wananchi wake. Pia uongozi unaendelea kupata ushirikiano mkubwa
sio tu ndani ya nchi bali na nje ya Tanzania. Hivyo tunaamini Tanzania
itaendelea kupiga hatua zaidi za kimaendeleo." Balozi Wang Ke.
Balozi huyo, kwa niaba
ya serikali na watu wa China amemuhakikishia Katibu Mkuu kuwa, wataendelea
kutoa ushirikiano wote kwa upande wa Serikali na Chama hasa kutokana na
historia nzuri iliyopo kati ya CCM na Chama Cha Kikomunisti cha China CPC.
Aidha, ametumia fursa
hiyo kuipongeza CCM kwa kuvuka salama, kwa amani na utulivu mkubwa katika
kipindi kigumu cha kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa
CCM Dkt. John Pombe Magufuli, na kufanikiwa kumpata mwenyekiti mpya na Rais wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo kwa
upande wa Katibu Mkuu kwa niaba ya CCM ameitumia fursa hiyo kumuomba Balozi
Wang Ke, kuendelea kuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini China kwa kuwa yeye
amepata bahati ya kuishi hapa, na kujionea mwenyewe utulivu na amani iliyopo
nchini.
Pia, Katibu Mkuu
amemuhakikishi Balozi kuwa, ushirikiano kati ya Tanzania na China, na kati ya
CCM na CPC sio wa kutiliwa mashaka, ni uhusiano wa kindugu na umejengwa katika
misingi ya kihistoria na kamwe hauwezi kutetereshwa.
Kikao hiko kimehudhuriwa
na baadhi ya viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
wakiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara Bi. Christina Mndeme, Katibu wa NEC,
Oganaizesheni Bi. Moudlin Cyrus Castico, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg.
Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Dkt. Hawasi Haule na Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania UWT Mwl. Queen Mlozi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment