Ameyasema hayo (Ijumaa, Januari 22, 2021) wakati akizungumza na makamanda na wadau mbalimbali mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.
Ujenzi wa chuo hicho ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Oktoba, 2020 wilayani humo wakati akimnadi aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli.
Waziri Mkuu alisema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni jembo jema katika idara ya uhamiaji na lina manufaa makubwa nchini. Alisema kuwa ujenzi wa majengo hayo ni muendelezo wa jitihada za Serikali za kuhakikisha idara hiyo inafanya kazi kwa ufanisi.
“Katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano, zipo jitihada kubwa zimefanywa za kuimarisha miundombinu kwenye majeshi yetu nchini, kwenye idara ya uhamiaji, tumewezesha upatikanaji wa nyumba 103 za makazi pamoja na ujenzi wa jengo la makao makuu mkoani Dodoma.”
Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya ndani ihakikishe inatenga mapema bajeti kwa ajili ya idara ya uhamiaji ili waweze kukamilisha miundombinu ya chuo hicho.
Waziri Mkuu pia aliipongeza idara ya uhamiaji kwa namna wanavyofanya kazi kwa weledi na kuibua mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahamiaji haramu wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu.
Naye, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Chilo amesema kuwa kambi hiyo ya mafunzo ya maafisa na maaskari wa idara ya uhamiaji ni matunda ya Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha jeshi la idara ya Uhamiaji.
Naibu Waziri Chilo alisema kuwa ujenzi wa kambi hiyo yenye ukubwa wa ekari 395, utasaidia wananchi wa maeneo ya jirani kupata huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji na umeme.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala amesema kuwa lengo kuu la kuanzisha kambi hiyo ya kijehsi ni kutoa mafunzo ya utayari kwa wakati na gharama nafuu, kupata askari wenye ukakamavu, nidhamu, weledi na maadili ya kikazi ya kiuhamiaji.
Dkt. Makakala alisema kuwa mpaka sasa wameshatumia sh. milioni 140 katika ujenzi zilizotokana na michango ya hiari ya maafisa na askari wa uhamiaji waliochangia sh. milioni 81 huku wadau mbalimbali wakichangia sh. milioni 59.
Alisema kuwa kambi hiyo kwa sasa ina uwezo wa kuchukua askari 300 kwa wakati mmoja na endapo watapata fedha, wanatarajia kuongeza uwezo wa chuo hadi kufikia askari wanafunzi 1,000.
Aidha, aliongeza kuwa idara hiyo inao mpango wa kuongeza majengo ya kudumu na kuwa na huduma muhimu za mabweni, zahanati, madarasa, nyumba za ibada na maktaba ili kukifanya chuo hicho kuwa na hadhi ya kitaifa na kimataifa. Alisema wanahitaji sh. bilioni 3 ili kutekeleza mpango huo.
Naye, Kaimu Meneja wa TANESCO mkoa wa Tanga, Bw. Juma Nkija alipoitwa aeleze ni lini umeme utafika chuoni hapo, alisema kuwa ndani ya siku tatu kuanzia kesho (Jumamosi, Januari 23, 2021) watawasha umeme katika transfoma na kama maandalizi ya majengo yatakuwa yamekamilika watawasha umeme katika majengo hayo. Pia alisema wana kazi ya kutenganisha mfumo wa umemejua (solar power) na umeme wa gridi.
Kuhusu suala la maji, Waziri Mkuu alimuita wa Maji Mkurugenzi wa Ufundi wa RUWASA, Mhandisi Deusdedit Magoma aeleze ni lini yatapatikana. Mhandisi Magoma alisema wamepokea sh. milioni 150 na kwamba ndani ya mwezi mmoja maji yatakuwa yanapatikana chuoni hapo.
“Vilevile kuna vijiji viwili pamoja na shule ya sekondari viko hapa jirani, wakati tukileta maji chuoni, tutahakikisha na vyenyewe vinapata maji,” alisema.
Mapema, Mbunge wa jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alipopewa nafasi asalimie, alimweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo lina shida kubwa ya maji na hata wakichimba wanaishia kupata maji yenye chumvi nyingi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Alisema zinahitajika sh. milioni 400 hadi 500 ili kufanikisha mradi wa kuvuta maji kutoka Parungu. “Mradi huu nashauri upite kwenye vijiji viwili vya jirani ambavyo viko umbali wa kilometa mbili na kwenye sekondari yenye wanafunzi wapatao 450 ili kuepusha bughudha kutoka kwa wakazi na wanafunzi ambao ni majirani halisi wa chuo hicho.”
0 comments:
Post a Comment