METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, January 29, 2021

WAZIRI KALEMANI ATOA MIEZI 6 KWA MKANDARASI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME LUGURUNI KUKAMILISHA UJENZI

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ametoa miezi 6 kwa Mkandarasi anayejenga kituo kipya cha Kupoza umeme Luguruni kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 28 Januari, 2021 alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho jijini Dar-e-salaam.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, Mradi mzima wa kujenga kituo hiki cha kupoza umeme Luguruni utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 15.2 na kuwa fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Waziri Kalemani amefafanua kuwa, ameamua kutembelea kituo hicho ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kutokana na umuhimu wake hasa kitakapokamilika.

Waziri Kalemani amesema, hapa nchini tunajenga vituo vingi sana vya kufua umeme ama kupoza umeme. “tumeshajenga vituo zaidi ya 134 mpaka sasa na tumekamilisha vituo vipya 24 hivi karibuni vikiwemo vya Singida, Rusumo, Nyakanazi na vingine na tunaendelea kujenga vituo vingine vya kupoza umeme zaidi ya 24 vipya ambavyo navyo vitakamilika ndani ya miezi sita hadi minane inayokuja” amesema Dkt. Kalemani.

Waziri Kalemani amesema, lengo la kujenga hivi vituo vya kupoza umeme, ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa kutosha, wa uhakika na unaotabirika wakati wote.

Waziri Kalemani amesema, Kituo cha Luguruni ni muhimu sasa. Amesema, kwa Dar-es-salaam peke yake na Pwani, hadi sasa tuna vituo takriban 11 vya kufua na kupoza umeme. Dkt. Kalemani amefafanua kuwa, vituo vya kupoza na kufua umeme kazi yake ni kuwafikishia watumiaji umeme wa uhakika na unaotabirika baada ya kutoka kwenye uzalishaji wake.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, pamoja na kuwa na tuna vituo vya Ubungo I, Ubungo II, Tegeta, Kunduchi, Ilala, Kurasini, Ilala na tunajenga Dege, lakini kituo hiki kilikosekana kwa muda mrefu.

Amesema, Kituo cha Luguruni ndio kituo muhimu sana kwa maeneo ya Dar-es-salaam kwa kuwa kinakwenda kuhudumia maeneo mengi zaidi. Dkt. Kalemani amesema, kituo cha Luguruni kitachocha na kupoza umeme ambapo laini ya kwanza itapeleka umeme maeneo ya maili moja mpaka kuelekea Chalinze na Mlandizi na laini ya pili itapeleka umeme maeneo ya Tegeta, kwenye Hospitali ya Mloganzila hospitali ya rufaa, ambayo ni hospitali muhimu sana.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, Hospitali ya Mloganzila ilikuwa inapata umeme kutoka Ubungo ambapo ni mbali sana na hivyo umeme uliokuwa unafika kwenye hospitali ya Mloganzila ulikuwa unafika tayari ukiwa hafifu.

Amesema Kituo hiki ni muhimu sana kwani kitapeleka umeme katika maeneo ya Mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam ikijumuisha Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, Msigani, Kibamba, Kibwegere, Kisarawe, Mail moja na maeneo ya viwanda. Waziri Kalemani ameongeza kuwa kukamilika kwa kituo cha Luguruni, kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo na kupunguza mzigo wa mashine nyingine za Ubungo, Songas na maeneo mengine mpaka Kinyerezi. “Kwa hiyo wananchi wa maeneo tajwa yatakayopokea umeme kutoka katika kituo hiki wataanza kupata umeme wa kutosha na wa uhakika ndani ya miezi sita kuanzia sasa.” Amesisitiza Dkt. Kalemani.

Waziri Kalemani ametoa rai kwa wananchi wote na wanaotoka nje ya nchi waje kuwekeza hasa katika maeneo ya Pwani kwa sababu kutakuwa na umeme wa uhakika na unaotabirika.

Dkt. Kalemani wito kwa Mkandarasi M/S (BEIJING) INDUSTIAL AND COMMERCIAL CO LTD kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ndani ya miezi sita.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 01 April, 2020 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2021 lakini Dkt. Kalemani amesema kwa kuwa tayari umeme umefika kwenye eneo la ujenzi, ametoa wito kwa Mkandarasi huyo kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi sita kuanzia  tarehe 28/02/2021.

Aidha, waziri kalemani amemtaka Mkandarasi huyo kuwaleta wafanyakazi wote wanaotakiwa kufanya kazi mahali hapo ili kuongeza kasi ya ujenzi wa kituo hicho. Aidha Waziri Kalemani ametaka vifaa vyote vilivyoko bandarini vinavyotakiwa kutoka ili vifanye kazi vitolewe kuwezesha kufanyika kwa kazi hiyo. Amewataka wakae na Bandari kwa mazungumzo na kukubaliana ili vifaa hivyo viweze kutoka na kutumika katika mradi huo.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa ni ufumbuzi wa tatizo la umeme kwa maeneo mengi ya jiji la Dar-es-salaam ikiwemo hospitali ya Mloganzila

Waziri Kalemani ametoa rai kwa wawekezaji na wadau waanze kuandaa miundombinu ya uwekezaji kwani umeme utakaopatikana Luguruni, utakuwa ni umeme mkubwa sana. Amesema kwa Dar-es-salaam pekee mashine zilizofungwa na zitakazofungwa, zitakuwa zimefungwa transforma zenye uwezo wa kuhudumia MW 1422 wakati matumizi ya umeme kwa Dar-es-salaam ni MW 400 - 520 hivyo bado matumizi ni kidogo ikilinganishwa na kiasi cha umeme kinachozalishwa.

Waziri Kalemani ameweka wazi kuwa, maeneo anayoona yana changamoto ni miundombinu ya nyaya na nguzo. Dkt. Kalemani ametoa wito kwa TANESCO kusimamia maeneo yote ya kurekebisha nyaya na nguzo na yafanyiwe kazi ndani ya miezi mitatu. “TANESCO simamieni Miundo mbinu hii” amesema Dkt. Kalemani.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com