METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, January 11, 2021

UWEPO WA REGISTA YA WATU WENYE ULEMAVU ITACHANGIA UPATIKANAJI WA HUDUMA BORA KWA WENYE ULEMAVU NCHINI – NAIBU WAZIRI UMMY

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (kulia) akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakati wa ziara yake mkoani humo alipokuwa amewarejesha baadhi ya wenye ulemavu kutoka Jijini Dar es Salaam kutokana na baadhi yao kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi kuomba fedha barabarani.

Baadhi ya washiriki wakisikiliza kwa makini maelezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (hayupo pichani) wakati wa ziara yake Mkoani Shinyanga.

Uwepo wa rejista ya Watu wenye Ulemavu nchini utachangia upatikanaji wa huduma bora kwa kundi hilo lenye mahitaji maalum sambamba na kutambua mahali wanapoishi, aina ya ulemavu walionao, hali zao za kimaisha na namna ya kuwawezesha kupata mikopo ya asilimia 2 inayotolewa na halmashauri.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati wa ziara yake ya kuwarejesha baadhi ya wenye ulemavu Mkoani Shinyanga kutoka Jijini Dar es Salaam, kutokana na kundi hilo kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi kuwazungusha watu wenye ulemavu kuomba fedha barabarani.

Alieleza kuwa, Serikali ipo katika mkakati wa kuandaa regista ya watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Halmashauri na Mkoa ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoonyesha idadi ya wenye ulemavu waliopo nchini na ambayo pia itasaidia kutambua kujua mahali walipo, wanajishughulisha na nini katika jamii waliyopo.

“Uwepo wa rehista hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa serikali kutambua idadi ya watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo mbalimbali na hivyo kurahisisha ufikikaji wa huduma kwa kundi hilo kwa urahisi,” alisema Naibu Waziri Ummy

“Leo hii tumewarejesha Watu wenye Ulemavu zaidi ya 38 kutoka Jijini Dar es Salaam kuja hapa Mkoani Shinyanga mahali ambapo wamekuwa wakiishi hapo awali, hivyo kama rejista hiyo ingekuwepo basi zoezi la utambuzi wa baadhi yao ingekuwa rahisi kuwatambua,” alisema

Alisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam walifanikiwa kufanya ziara za kushtukiza katika maeneo ambayo wamekuwa wakiifadhiwa watu hao wenye ulemavu, wakati wa operesheni hiyo walifanikiwa kuwakamata baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumika kuwaendesha wenye ulemavu kuomba fedha barabarani, wamiliki wa nyumba hizo za wageni ambazo wamekuwa wakihifadhi wenye ulemavu na pia walifanikiwa kukamata vitimwendo “wheelchair” ambazo zilikuwa zikikodhishwa kwa watu wenye ulemavu.

“Tutaendelea na msako hadi pale tutakapoona wahusika wa mtandao huu wanaacha kabisa vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu,” alisisitiza Naibu Waziri Ummy

Aliongeza kuwa, Serikali hii ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli inawajali sana Watu wenye Ulemavu na katika kulitambua hilo Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kundi hilo linapata mahitaji wanayostahili kama watu wengine.

Sambamba na hayo Naibu Waziri Ummy alitaka Uongozi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine iliyopo nchini kuhakikisha wanawasaidia watu wenye ulemavu kuanzisha miradi mbalimbali itakayowafanya wajishughulishe na uzalishajimali badala ya kuzunguka barabarani kuomba fedha.

“Nilipofanya ziara ya kuwatembelea watu wenye ulemavu mkoani Dar es Salaam nimeshuhudia mambo makubwa yanayofanywa na baadhi yao ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya uzalishaji, ujasiriamali, hivyo wenye ulemavu watambue wanao uwezo wa kuanzisha miradi mikubwa,” alisema  

Aidha, Naibu Waziri huyo aliwasihi Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu na wateja wengine kwa kufuata miongozo, kanuni na Sheria zinazoongoza katika utoaji wa huduma za ustawi wa jamii nchini. Pia amewataka maafisa hayo kuimarisha ushirikiano baina yao na watu wenye ulemavu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Yasinta Mboneko alikiri kuwapokea watu hao wenye ulemavu ambao walikuwa wakitumiwa na baadhi ya watu kujinufaisha, huku akieleza kuwa wataanzisha kanzi data kwa ajili ya kuhifadhi taarifa ya watu wenye ulemavu waliopo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo pia alimuhakikisha Naibu Waziri kuwa watawarejesha salama mahali walipokuwa wanaishi huku wakiweka utaratibu wa kuwafuatilia.

Mhe. Mboneko alitumia fursa hiyo kukemea vitendo hivyo kwa baadhi ya watu ambao wanawatoa wenye ulemavu na kuwapeleka kwenye baadhi ya miji kuomba huku akieleza mtu yoyote atakayebainika anafanya vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.  

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com