Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mkoani Njombe Wakili Joseph Kamonga ameshauri Serikali kufuta leseni za Wamiliki wa Vitalu vya Madini Wilayani Ludewa ambao hawafanyii kazi Maeneo hayo ili kutoa nafasi kwa Wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuyaendeleza.
Alitoa ushauri huo Januari 09/2021 kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Njombe, baada ya kupata Taarifa kutoka Ofisi ya Madini Mkoani hapa kuwa Wilaya ya Ludewa ina jumla ya leseni 201 za umiliki wa maeneo ya Madini lakini kati ya hizo zinazofanya kazi ni tano pekee.
“Naishukuru Ofisi ya Madini Mkoa wa Njombe kwa kuweka data hizi hadharani, tumeambiwa Wilaya ya Ludewa zipo leseni za Madini 201 lakini zinazo fanya kazi ni tano pekee, nashauri leseni hizi zifutwe bila kujali mmiliki ni nani ili kutoa nafasi kwa Wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuyafanyia kazi maeneo haya” Alisema Kamonga.
Kupitia Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya, Mbunge wa Ludewa Wakili Kamonga alimwomba kumfikishia Ombi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli ili Miradi ya Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe Nchuchuma Wilayani Ludewa ianze kufanya kazi na kutoa Fursa ya Uchumi kwa Jamii.
Andrea Tsere Mkuu wa Wilaya ya Ludewa alisema kuna maeneo yapo nje ya Miradi ya Liganga na Nchuchuma Wilayani humo ambayo yalipaswa kumilikiwa na Wachimbaji wadogo lakini yamechukuliwa na NDC na kuwanyima Fursa Wachimbaji hao jambo ambalo linapaswa kutazamwa ili NDC wayaachie na kutoa fursa kwa Wachimbaji wadogo.
“Katika Miradi ya Chuma na Makaa ya Mawe Wilayani Ludewa kuna maeneo yapo nje ya Miradi hii lakini yapo chini ya NDC, Ombi langu hawa NDC wayaachie ili wapewe Wachimbaji wadogo ambao wanauhitaji wa kufanya kazi na kutoa fursa kwao na Serikali” Mhe, Andrea Tsere Mkuu wa Wilaya ya Ludewa.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya alisema Serikali inaendelea kupitia Mkataba wake na Mwekezaji ambao unampa faida zaidi Mwekezaji kuliko Serikali hata hivyo Ofisi yake itawasilisha Ombi kwa Rais Magufuli la kuanza kuifanyia kazi Miradi hiyo.
Aliongeza kuwa Ofisi yake itazungumza na Shirika la Maendeleo Nchini NDC liwaachie Wachimbaji wadogo baadhi ya Maeneo yaliyopo nje na Miradi ya Chuma na Makaa ya Mawe Wilayani Ludewa, waweze kufanyia kazi huku akibariki uamuzi wa kuzifuta leseni ambazo kwa muda mrefu hazifanyi kazi na kuishia kumiliki maeneo bila faida.
0 comments:
Post a Comment