METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, December 19, 2020

WAZIRI MHAGAMA: “Wastaafu walipwe mafao kwa wakati kupunguza malalamiko”

Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa kufunga semina ya wajumbe wa Shirikisho la Mashirika  ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) walipokutana tarehe 19 Desemba, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hotel ya Gold Crest Jijini Mwanza.Mkutano ulihudhuriwa na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini (TSSA) Bw. Meshack Bandawe,akizungumza kuhusu shirikisho la Mifuko hiyo wakati wa mkutano wao mara baada ya kuhitimisha mafunzo ya siku Tatu mkoani Mwanza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameitaka mifuko ya Hifadhi ya jamii kulipa mafao ya wanachama wao kwa wakati ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima.

Ametoa kauli hiyo Desemba 18, 2020 alipokuwa akifunga semina ya siku tatu iliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) na kuhudhuriwa na  Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo.

Waziri alieleza, upo umuhimu wa kila mfuko kuona tija ya kulipa wanachama wao kwa wakati ili kuondokana na usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wale wenye sifa za kulipwa na kusaidia wanachama hao kukidhi mahitaji yao kwa wakati mwafaka.

 “Ni lazima kuhakikisha kuwa wanachama wanalipwa mafao yanayoendana na wakati ili kuwawezesha kukidhi matarajio yao bila kusahau wana mchango mkubwa katika mifuko yetu”. alieleza waziri

Alifafanua kuwa, amekuwa akipokea malalamiko mengi kwa wastaafu kuhusu ucheleweshwaji wa mafao yao, hivyo kuonesha viashiria vya udhaifu kiutendaji na kuzielekeza mamlaka husika kutatua changamoto hiyo kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.

Aliongezea kuwa, mifuko inawajibu mkubwa wa kuhakikisha Waajiri wanaandikishwa na wanalipa michango kwa wakati.Idadi ya Waajiri ambao hawalipi michango imeongezeka hususan makampuni ya Ulinzi.

“Mifuko ipunguze usumbufu usikuwa wa lazima kwa wanachama hasa baada ya kustaafu na kudai mafao, kwa mfano mwanachama anastaafu akiwa na miaka 60 anaanza kudaiwa nyaraka ambazo aliwasilisha wakati anasajiliwa, kama kuna mabadiliko ya taarifa zinatakiwa zifanyiwe kazi na maafisa matekelezo kabla mwanachama kustaafu,”alisisitiza Waziri Mhagama  

 

Aidha alieleza kuwa Azma ya Serikali ni kuona Watanzania wote wenye uwezo wa kufanyakazi wana andikishwa katika Mifuko ya Pensheni maana  takwimu zinaonyesha bado kuna idadi kubwa ya wafanyakazi katika Sekta rasmi na isiyo Rasmi ambao bado hawajaandikishwa.

 

“Kwa kuangalia takwimu zilizopo, hadi sasa kuna jumla ya wafanyakazi walio andikishwa na kuchangia katika Mifuko  kwa idadi ndogo, mfano mfuko wa NSSF wapo  543,889 na PSSSF ni 627,097 ambapo idadi hiyo ni sawa na 4.3% ya nguvu kazi (Labour Force). Hivyo kazi kubwa inatakiwa kufanyika hususan katika Sekta isiyo rasmi,”alisema

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) Bw.William Erio alipongeza jitihada za Waziri katika kuratibu na kusimamia shughuli za mifuko iliyochini ya ofisi yake na kuahidi kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa pamoja na kuhakikisha wanakuwa na mikakati thabiti ya kushiriki katika miradi ya kimkakati ya Serikali ili kuwa na tija katika Taifa.

Aliongezea kuwa, wana lenga kuhakikisha wanaboresha huduma zao kwa wanachama na kuwafikia kwa wakati ili kuendelea kunufaika na uwepo wa mifuko nchini.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com