METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, December 24, 2020

Waziri Bashungwa aiagiza Kamisheni ya Ngumi kuboresha Utendaji Kazi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu   Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo leo Desemba  24, 2020 wametembeleaa kambi za mazoezi za  mabondia Abdallah Shabani Pazi (Dulla Mbabe)  iliyoko Mwananyamala  Dar es Salaam  na Mfaume Mfaume  iliyoko Manzese Dar es Salaam na kuwatakia heri katika Mpambano yao ya kimataifa yatakayofanyika Desemba 26, 2020 Next Door Arena, Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameiagiza Kamisheni ya Ngumi nchini kuimarisha utendaji wake ili ulete mafanikio zaidi katika mchezo wa Ngumi za kulipwa. 

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 24, 2020, Jijini Dar es Salaam alipowatembelea mabondia Mfaume Mfaume na  Abdallah Shaban Pazi maarufu  kwa jina la Dulla Mbabe  katika kambi zao za mazoezi kuelekea mapambano ya kimataifa   yatakayofanyika Desemba 26, 2020 Ukumbi wa Next Door Arena, jijini Dar es Salaam. 

Katika ziara hiyo Mhe. Bashungwa ametoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kujitokeza   kudhamini mchezo huo wa masumbwi ambao umekua miongoni mwa michezo inayotangaza nchi vizuri. 

"Kwenye Sekta ya Michezo hatutarudi nyuma katika kuiendeleza, na katika hili vyama au mashirikisho ya michezo ambayo hayatatekeleza majukumu yake hatutasita kuwachukulia hatua ikiwemo kuvifuta" alisema Mhe. Waziri Bashungwa. 

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo kurasimisha maeneo yote ya kufanyia mazoezi (GYM) pamoja na kuyasajili ili   yatambulike.                      

"Vipaji vingi vipo tunahitaji kuviendeleza, kwa kuwa ni ajira na njia ya kupata kipao" alisema Mhe. Ulega. 

Naye Bondia Abdallah Shaban Pazi (Dallah Mbabe) ameishukuru Serikali kwa kutambua mchezo wa ngumi kama njia ya ajira na kuiwekea mazingira bora, huku akiahidi kupata ushindi. 

Vilevile Bondia Mfaume Mfaume amesema kuwa amejipanga kufanya vizuri katika pambano hilo ili kuiletea nchi heshima.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com