METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 13, 2020

VIONGOZI, WANANCHI NA WADAU SIMIYU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUKAMILISHA UJENZI WA MADARASA

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.  Anthony Mtaka amewataka viongozi wa kisiasa kushirikiana pamoja na viongozi serikali na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha ujenzi wa madarasa unakamilika mapema, lengo likiwa kuhakikisha wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanapata madarasa ya kusomea.
 

Mtaka ameyasema hayo  Desemba 12,2020 kwenye kikao kazi cha mkoa cha kujadili uelekeo wa mkoa wa Simiyu katika kipindi cha miaka  mitano ijayo  (2020/2025 ) katika masuala mbalimbali ikiwemo afya,elimu,kilimo,viwanda na ajira kwa vijana, ambacho kimewashirikisha viongozi wa chama na serikali, ,wafanyabiashara ,viongozi wa dini ,taasisi za umma na binafsi na wadau wa maendeleo wa Mkoa, kilichofanyika Mjini Bariadi mkoani Simiyu.

 

“Simiyu kipaumbele chetu cha kwanza ni elimu, nimekuwa nikiwaambia watu wa Simiyu tukitaka kushindana tusomeshe watoto, malizieni maboma ya madarasa watoto wapate mahali pa kusomea, kila mmoja abebe kwa uchungu jambo hili kuona madarasa yanakamilika lakini mkienda  kwenye mabaraza mkaanza kubishana hamtawasaidia wananchi,” alisema Mtaka

 

Aidha Mtaka ameongeza kuwa kwa maeneo ambayo yana madini pamoja na maeneo yanayonufaika na uhifadhii kama vile vijiji vya Makao, Mwangudo na vingine Wilayani Meatu, wananchi wasichangishwe badala yake asilimia zinazotolewa kwa ajili ya vijiji zielekezwe kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa.

 

 Ameongeza kuwa mkoa huwa umejiwekea malengo ya kuongoza katika mitihani yote ya Taifa ambapo amewataka viongozi wa Serikali kuendelea kutoa motisha kwa walimu ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa lugha za kuwaudhi na kuwakera walimu ili waendelee kufanya kazi kwa moyo.

 

Sambamba na hili Mtaka ametoa rai kwa Madiwani wote wa Mkoa huo kuacha tabia ya kuazimia watumishi wao kwa kuwa hali hiyo inawavunja moyo watumishi badala yake waweke mazingira ya watumishi kupenda kazi na ikiwa watumishi watafanya jambo lisilotakiwa wawasiliane na mamlaka nyingine ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu.

 

Katika hatua nyingine Mtaka amesema Simiyu Imejipanga kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo nafuu itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa kwa vijana wanawake na walemavu, akibainisha kuwa fedha hizo zitatangazwa na kushindaniwa; ambapo vikundi havitapewa fedha badala yake Halmashauri zitalipia teknolojia zinazohitajika kupitia SIDO na sehemu ya fedha inayobaki itatumika kuwajengea uwezo wahusika wa vikundi hivyo.

 

Awali akitoa taarifa ya elimu mkoani hapo kwa niaba ya afisa elimu mkoa wa Simiyu , Jusline Bandiko  amesema mkoa huo una mahitaji ya vyumba vya madarasa 565 ,vilivyopo ni 419 huku  upungufu ukiwa vyumba 155 ambavyo vinatakiwa  kukamilika kwa ajili ya kidato cha kwanza 2021.

 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simyu, Mhe. Enock Yakobo ametoa wito kwa viongozi kuona umuhimu wa kuanzisha mfuko wa elimu wa mkoa na kuwahamasisha wananchi kuchangia mfuko huo ili uweze kusaidia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na ununuzi wa viti na madawati.

 

Miriam Mmbaga ni Katibu Tawala wa Mkoa huo ametoa wito kwa viongozi wa Umma mkoani Simiyu kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo, sheria na taratibu na kwa uadilifu mkubwa wakijiepusha na masuala ya migongano ya maslahi katika maeneo yao, huku akisisitiza wafanye maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwa maslahi ya wananchi wanaowaongoza.

                               

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James ambaye pia ni Mlezi wa CCM kwa mikoa ya Simiyu na Mara  amesema jamii inahitaji mageuzi ili kufikia mageuzi hayo inapaswa kuwa na viongozi wenye uthuhutu na ujasiri, huku akitoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu kufanya kazi kwa ushirikiano na kutumia vizuri madaraka, mamlaka na ushawishi walio nao kwa manufaa ya wananchi wanaowaongoza.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com