Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo kuhusu maendeleo ya uzalishaji wa mbegu bora pamoja na miche ya michikichi leo tarehe 17.12.2020 katika ziara yake katika Kituo mahiri cha utafiti wa zao hilo (TARI Kihinga) mkoani Kigoma.
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo kuhusu mifuko
maalum ya kuoteshea miche bora ya michikichi, leo tarehe 17.12.2020 katika
ziara yake katika Kituo mahiri cha utafiti wa zao hilo (TARI Kihinga) mkoani
Kigoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald
Kusaya amesema Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo
(TARI – Kihinga) imefanikiwa kuzalisha mbegu bora milioni 4 za zao la chikichi
kama sehemu ya mkakati wa kuokoa fedha za Serikali wa kutumia zaidi ya shilingi
bilioni 443 ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya
nchi.
Katibu Mkuu Kilimo Bwana Kusaya
ameyasema hayo leo tarehe 17.12.2020 wakati wa ziara yake ya siku tatu ya
kutembelea, kukagua na kujionea shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo mkoani
Kigoma ambapo leo ametembelea Kituo mahiri cha utafiti wa zao la chikichi (TARI
Kihinga) katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Katibu Mkuu Kusaya amesema hadi kufikia
tarehe 10 Desemba, 2020 Kituo cha TARI Kihinga kimezalisha zaidi ya mbegu bora
4,205,335 za zao la chikichi na zimetolewa kwa Halmashauri sita za mkoa wa
Kigoma; Zinazolima zao hilo.
Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa
ya Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya
Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.
Katibu Mkuu Kusaya amesema mahitaji ya
mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 kila mwaka ambapo uwezo wa nchi kuzalisha
ni tani 205,000 sawa na asilimia 36% na kuongeza kuwa kiasi cha tani 365,000
sawa na asilimia 64 ya mafuta huagizwa toka nje na kuigharimu nchi kiasi cha
shilingi biloni 443 kila mwaka.
Katibu Mkuu Kusaya amesema ili
kukabiliana na changamoto hiyo Wizara iliona ni vyema kuanza na uzalishaji wa
mbegu bora.
“Uwezi kukabiliana na changamoto ya
namna hiyo bila ya kuanza na mbegu; Ndiyo maana tumeona tuanze na mbegu bora
kwanza; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
alitoa maelekezo ya kuondokana na utegemezi huo tarehe 28 Julai, 2018 baada ya
kufanya kikao na Wadau ili kuweka mkakati wa upatikanaji wa mafuta ya kula
nchini kupitia uendelezaji wa zao la chikichi.”
“Mojawapo ya mkakati ni kuongeza
upatikanaji wa mbegu bora za michikichi zinazotoa mafuta mengi kuliko
zinazolimwa sasa.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Serikali imeamua kuanza na mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa zaidi ya mikoa 16
imeonyesha kuwa na fursa ya kupanda zao la chikichi.
Katibu Mkuu Kusaya ametoa wito kwa
Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma kuendelea kuzalisha miche milioni moja
kupitia mbegu bora hizo zilizozalishwa na kutolewa na Kituo cha TARI Kihinga na
ameendelea kuhimiza ushirikiano katika ya Halmashauri hizo na Kituo hicho.
Katika Taarifa yake kwa Katibu Mkuu Kilimo
Gerald Kusaya Msimamizi wa Kituo cha TARI Kihinga Dkt. Filson Kagimbo amesema
hadi sasa kiasi cha mbegu 1,863,111 zilishatolewa kwa Taasisi nyingine za Umma
na Sekta Binafsi.
Amezitaja Taasisi hizo ni pamoja na
TARI Kihinga yenyewe (120,000), JKT Bulombora (219,691), Gereza la Kwitanga
(286,125), Gereza la Ilagala (15,795), Shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo, ASA
- Bugaga (50,000), Taasisi ya Utafiti Ilonga – TARI Ilonga (235,500) na Sekta
Binafsi mbegu (936,000). Baada ya Taasisi hizo kupewa mbegu hizo ambapo jumla
ya miche 1,087,143 imezalishwa.
Dkt. Kagimbo ameongeza kuwa Jumla ya
Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma zilipewa kiasi cha mbegu 306,000 ambapo
jumla ya miche 183,175 ilizalishwa. Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya
Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya
Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.
Wakati huo huo katibu Mkuu Kusaya
amekabidhi trekta kama sehemu ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mbegu
bora pamoja na miche kwa kituo cha TARI Kihinga. Trekta hilo lenye thamani ya
shilingi milioni 75 limekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi
za Taasisi hiyo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa hadi
sasa Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya
kuendeleza zao la chikichi kupitia Kituo cha TARI Kihinga.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo (TARI Makao Makuu) Dkt. Geoffrey Makamilo amemshukuru Katibu
Mkuu kupitia Wizara ya Kilimo kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh 1,457,952,000 kwa
ajili ya kuzalisha mbegu na kuimarisha miundo mbinu ya TARI Kihinga pamoja na
ununuzi wa gari la Watumishi pamoja na ununuzi wa trekta hilo pamoja na zana
zake.
0 comments:
Post a Comment