Baadhi ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Lubaga uliopo mpakani mwa Wilaya ya Bariadi na Busega, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) alipotembelea mgodi huo akiwa na viongozi wa Chama na Serikali mkoani humo Desemba 17, 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesitisha matumizi ya leseni 18 za uchimbaji madini katika mgodi wa Dhahabu wa Lubaga uliopo mpakani mwa wilaya ya Bariadi na Busega, mpaka pale zitakapotolewa ufafanuzi na Waziri mwenye dhamana ya madini juu ya uhalali wake katika uendeshaji wa shughuli za madini.
Mtaka ametoa uamuzi huo katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika eneo la mgodi Desemba 17, 2020 akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kwa ajili ya kwenda kusikiliza kero za wachimbaji wadogo mgodini hapo na kuzitafutia ufumbuzi.
“Sisi kama viongozi wa mkoa tunasitisha matumizi ya leseni za eneo lote hili, mpaka pale waziri mwenye dhamana atakapokuja kutoa ufafanuzi kwa wananchi, kwa sababu sheria inamtamka waziri kwenye kufuta leseni lakini sisi mkoa kwa tuliyoyaona hapa tunasitisha; kwa sasa mgodi utaendelea kuwa chini ya usimamizi wa maelekezo ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema Maafisa kutoka katika Ofisi zote zinazopaswa kutoa huduma kwa wachimbaji hao ikiwa ni pamoja na maafisa wa Soko la Madini kuanzia Desemba 18, 2020 watakuwa katika eneo la mgodi ili kuwapunguzia wachimbaji hao adha ya kufuata huduma mbali na eneo hilo huku akisisitiza wachimbaji hao wauze dhahabu kwa bei iliyopo sokoni.
Mtaka pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Bariadi na Busega kufanya tathmini ya mashamba yaliyoharibiwa na shughuli zinazoendelea katika eneo la mgodi ili wakulima hao waweze kulipwa fidia, huku akiwataka Wakurugenzi hao pia kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa matundu ya vyoo yasiyopungua 12 kuimarisha hali ya usafi mgodini.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa onyo kwa wachimbaji na watu wote wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji madini kujiepusha na utoroshaji wa dhahabu, kwamba watakapobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha dhahabu hiyo.
Awali wachimbaji wadogo, wamiliki wa mashamba na wamiliki wa maduara waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye mgodi huo ambazo baadhi zilipatiwa ufumbuzi na uongozi wa mkoa na baadhi zitashughulikiwa na Waziri mwenye dhamana ya madini.
“Usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kwenye mgodi huu uimarishwe zaidi, ili Serikali ipate sehemu yake, wachimbaji na sisi tupate sehemu yetu na kila tozo au ushuru wanaotutoza wahakikishe wanatoa risiti za kielektriniki,” alisema Flugence Ekondo mchimbaji mdogo.
“Katika ugunduzi wa mgodi huu mke wangu alikuwa anapalilia mahindi akaokota jiwe, alivyolileta tulikuwa na wasiwasi nalo tukalipeleka mgodi wa Gasuma tukaambiwa ni dhahabu, hiyo ilikuwa tarehe 05/11/2020 kesho yake wachimbaji wakaanza kuchimba na mgao ukafanyika; binafsi nilijua hiyo itakuwa rashi itakayotunufaisha wachimbaji wadogo na jamii inayotuzunguka,lakini baadaye tukasikia kuna leseni tunaomba tusaidiwe na sisi tupate haki yetu kwenye mgao,” Ntimba Masalu mwakilishi wa wenye mashamba
Akitoa ufafanuzi kuhusu mgao, Afisa madini Mkazi wa Mkoa, Mhandisi. Oscar Kalowa amesema “katika mifuko 100 asilimia saba ni fedha ya serikali, wamiliki wa mashamba asilimia 15, msimamizi/mmiliki wa leseni asilimia 15 na mwenye duara husika anapata asilimia zinazobaki na huu ndiyo utaratibu unaohusika.”
0 comments:
Post a Comment