Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais - Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah mara baada ya kufanya mazungumzo baina yao, ambapo Mhe. Ummy alikwenda Ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Dkt. Khalid Salum Mohammed.
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais - Zanzibar
Mhe. Hemed Suleiman Abdallah alipofika Ofisini kwake kwa lengo la
kujitambulisha. Wengine katika picha ni Balozi Mbarouk Mbarouk Mkurugenzi Idara
ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais.
Makamu wa Pili wa Rais - Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah amesema ni vema changamoto za Muungano zinapojitokeza zipatiwe ufumbuzi wa haraka kupitia kupitia vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Ameyasema hayo wakati wa kikao baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu aliyefika Ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha.
Makamu wa Pili wa Rais - Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah amempongeza Waziri Ummy Mwalimu kwa kuteuliwa tena na kumhakikishia kumpa ushirikiano katika kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa mustakabali wa Taifa letu.
“Naamini kuletwa katika Wizara hii utapata fursa nzuri ya kusimamia masuala ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali na Taasisi zetu kwa maslahi ya watanzania wote, nina imani kubwa na utendaji wako, sina shaka kabisa” Alisisitiza Mhe. Hemed Abdallah.
Kwa upande wake Mhe. Ummy Mwalimu amesema anadhamana ya kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira na amesisitiza kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais pia kwa mambo yasiyo ya Muungano na kutolea mfano eneo la Mazingira hususan changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi, tatizo linalokabili dunia kwa sasa.
“Napenda kukuhakikishia kuwa nitafanya kazi kwa karibu na Dkt. Khalid Waziri mwenzangu katika kuhakikisha tunaimarisha Muungano wetu na kuendelea kushirikiana hata katika masuala ya mazingira kwa kuwa hayana mipaka” Alisisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy Mwalimu yuko Visiwani Zanzibar kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo hii leo atatembelea miradi ya Muungano inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano.
0 comments:
Post a Comment