METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 12, 2020

MSANJILA AFUNGUA FURSA KWA KAMPUNI YA AGA BULLION KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA MADINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini akizungumza jambo wakati alipokutana na watendaji wa kampuni ya AGA Bullion Novemba 12, 2020 Jijini Dodoma
Picha ya Pamoja ya Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila akizungumza na watendaji walipokutana Novemba 12, 2020 Jijini Dodoma

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila leo Novemba 12, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na kampuni ya AGA Bullion kutoka Nchini Uturuki iliyoonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini Nchini. .

Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, Katibu Mkuu Msanjila ameileza kampuni hiyo uwepo wa Masoko ya Madini yaliyoanzishwa kila mkoa nchini hususani ile yenye uzalishaji mkubwa wa madini ikiwa ni pamoja na mkoa wa  Geita, Mwanza, Kahama na Chunya, Arusha na kwingineko  ambako AGA Bullion wataweza kuwekeza, kununua na kuuza  dhahabu kwenye masoko ya nje.  

Prof. Msanjila ameitaka kampuni ya AGA Bullion kuwafikia wachimbaji wadogo na wa kati kwa kuwapa uzoefu wa uwekezaji katika sekta ya madini na kupendekeza kutembelea Mgodi wa dhahabu wa Geita na Busolwa, mgodi wa kati unaofanya uwekezaji katika uchimbaji wa madini ya dhahabu vizuri nchini.

Amesisitiza Uwekezaji unaopangwa kufanywa na  kampuni ya AGA Bullion usilenge  kwenye biashara ya madini ya dhahabu pekee bali kwenye madini mengine yanayopatikana nchini yakiwemo  madini ya Tanzanite yanayopatikana mkoani Manyara,  pia  kuomba  leseni ya uchimbaji  ili waweze kuchimba  madini  nchini.

Prof. Msanjila ameitaka Kampuni ya Aga Bullion kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya Madini  wakiwemo  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao hutoa huduma na ushauri wa kitaalam kwa wachimbaji wadogo, uchenjua dhahabu, kununua na kuuza kutokana na uwepo wa Refinery mkoani Mwanza itakayoanza shughuli mwezi Disemba, 2020. Taasisi ya jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kupata taarifa za kitafiti ndani ya nchi, ramani za kijiolojia zinazoonyesha sehemu zenye madini na Tume ya Madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwanzilishi wa AGA Bullion, Sarp Tarhanaci amemweleza  Prof. Msanjila kuwa Kampuni ya Aga Billion inamiliki viwanda viwili vya usafirishaji wa dhahabu (Refineries) katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (Dubai) na Uturuki, Pia, ameelezea uzoefu wao  katika ununuzi wa dhahabu kutoka katika mataifa mbalimbali kama vile Ghana, Burkina Faso, Peru, Malaysia na Uturuki.

Akizungumzia juu ya maelekezo ya kukutana na wadau wengine wa Sekta ya Madini, Tarhanaci amesema tayari kampuni hiyo tarehe 10/11/2020 ilikutana na kufanya mazungumzo na Tanzania Chambers of Mines (TCME), (Chama cha wachimbaji wakubwa wa Madini)  ambapo imepokea taarifa za uzalishaji na mauzo ya dhahabu, Tarehe na 11/11/1010 ilikutana na Mkurugenzi wa Masoko ya Kifedha  wa Benki Kuu ya Tanzania ili kueleza nia yake ya kutaka kutoa huduma ya usafirishaji wa dhahabu, bima na kutafuta masoko ya kimataifa ya dhahabu iliyosafirishwa kwa gharama ya 0.5% hadi 0.8% ya thamani ya madini hayo.

Aidha amesema, kampuni ya AGA Bullion kwa kiasi inayo dhamira ya kufanya biashara ya madini ya dhahabu kutoka wa wachimbaji wadogo,  wachimbaji wa kati ikiwemo kuwawezesha kwa kuwapa mitaji ya fedha ili waweze kuzalisha zaidi na kutoa mafunzo kwa wachimbaji, na kukutana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA)  ili waweze kujadili mambo mbalimbali kwa pamoja.

Aidha amezungumzia nia ya kampuni hiyo kusaidia kiwanda vya uongezaji thamani madini ya dhahabu (jewellery industry) kwa kutengeneza bidhaa zake kama vile pete, hereni na mikufu.

Viongozi wengine waandamizi wa wizara waliohudhurio Kikao hicho ni pamoja na Kamishina wa Madini, Muhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Issa Nchasi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com