METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 11, 2020

WAZAZI, WALEZI WAPUNGUZIENI KAZI WANAFUNZI WA MADARASA YA MITIHANI: RC MTAKA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania-TIC, Dkt. Maduhu Kazi (wa tatu kulia) akikata utepe kufungua chuo cha  ufundi Kasoli  iliyojengwa  kwa msaada na Mwekezaji wa Kampuni ya Alliance Ginnery na baadaye kukabidhiwa kwa Serikali jana  katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Sehemu ya majengo ya chuo cha  ufundi Kasoli  iliyojengwa  kwa msaada na Mwekezaji wa Kampuni ya Alliance Ginnery na baadaye kukabidhiwa kwa Serikali iliyopo  katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapunguzia kazi  wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani ya Taifa (darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne) ambayo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ili waweze kujipatia muda mwingi wa kujisomea kujiandaa na mitihani hiyo.

 

Mtaka ameyasema hayo jana  wakati makabidhiano ya Chuo cha Ufundi Kasoli katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi kilichojengwa na mwekezaji Alliance Ginnery Limited na kukabidhiwa kwa Serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi kwa niaba ya kampuni hiyo na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa niaba ya wananchi.

 

“Darasa la saba wameshafanya mtihani wao, watoto wa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne waendelee kufanya maandalizi, wazazi na walezi wapunguzieni kazi watoto wote walio kwenye madarasa haya na wakiwa nyumbani wafanye majadiliano ya pamoja,” alisema Mtaka.

 

Aidha, Mtaka amewaonya wazazi na walezi wenye nia ya kuwaozesha wanafunzi wa kike waliohitimu elimu ya msingi kuwa watakaofanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, huku akitoa wito kwa jamii yote kuwa walinzi wa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

 

Mtaka ameishukuru Kampuni ya Allience Ginnery kujenga chuo cha ufundi Kasoli na kutoa wito kwa wasichana na wanawake kijiji cha Kasoli kujitokeza kupata mafunzo ya ushonaji bila malipo katika chuo hicho katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, kabla ya kuanza kwa mafunzo yatakayoanza mwakani kwa mtaala wa Serikali na kuahidi kutoa vyerehani 25.

 

Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola amesema Kampuni hiyo imekuwa inajihusisha sana na maendeleo ya jamii katika sekta ya elimu, afya na maji kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii, ni wajibu wao  kufanya hivyo na ni sehemu ya maelekezo ya TIC wanayopewa wawekezaji wote.

“Tunashiriki kwenye masuala ya jamii kwa sababu sisi ni sehemu ya jamii, sisi tunashughulika na wakulima na wanaotulimia pamba na kutuuzia kutuwezesha kuendesha kiwanda chetu, siku za nyuma tulijikita kwenye afya, maji na elimu ya msingi na sekondari; tumeona haja ya kujenga chuo cha ufundi ili wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na masomo, wapate mafunzo  ya ufundi ili waweze kujitegemea,” alisema Ogola.

Aidha, Ogola amesema pamoja na mafunzo ya ufundi mipango ya baadaye ya kampuni ya Alliance Ginnery kuongeza darasa moja la wakulima kwa lengo la kutoa warsha na mafunzo kwa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija ili kampuni hiyo iweze kupata malighafi bora kwa ajili ya kiwanda chake cha kuchambua pamba..

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kujenga chuo cha Ufundi na kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao huku akiahidi kuwa TIC itahakikisha kinakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.

 

 “TIC inashirikiana na Serikali hata ngazi ya mikoa na tumejielekeza zaidi kuongeza ufanisi katika shughuli zetu za kuwasaidia wawekezaji masuala ya vibali kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika; pia tumejipanga hata kuwafikia wawekezaji wadogo Watanzania maana baada ya tathmini tumeona eneo hilo kuna mapungufu maana wengi wanadhani sisi tunahusika na wawekezaji wa kigeni tu,” alisema Dkt. Kazi.

Naye Mkazi wa Kijiji cha Kasoli Shamsa Abdallah amesema anaishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kwa kuwajengea chuo cha ufundi na anaamini kuwa kitawasadia kwenye mafunzo ya ushonaji  na mafunzo yanayohusiana na kilimo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kampuni ya Alliance Ginnery Limited imejenga majengo ya chuo cha ufundi Kasoli kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 180, kuchimba kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa pamoja na kuweka vifaa kama vyerehani, majiko ya gesi  na vifaa mbalimbali vya kujifunzia upishi,vifaa vya kujifunzia uashi na useremala meza na viti vya ofisi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com