METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 3, 2020

WANANCHI WAFURAHIA UPATIKANAJI WA MAJI

Wananchi wafurahia upatikanaji wa maji safi na salama ambapo wameaswa kuilinda na kuitunza miradi ya maji iliyopo na itakayoanzishwa kwa manufaa ya sasa na ya baadae kwani maji ni uhai, maji ni maisha.

Hayo yamebainishwa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya maji kwenye Tarafa yake ambayo imesaidia kupunguza tatizo la maji.

"Serikali ya Rais Magufuli inajitahiti kuleta huduma za maji mpaka maeneo ya vijijini inayoleta furaha kwa jamii. Leo nimetembelea miradi ya maji kwa kata mbili tu, nimejionea ilivyo mkombozi wa kero ya maji iliyokuwepo awali. Wananchi wanaendelea kunywa maji safi na salama yanayopatikana muda wote. Niwaase miradi hii ya maji itunzwe vyema kwa manufaa ya sasa na ya baadae" alisema Gavana Shilatu.

Tatizo la maji ilikuwa kero kubwa kwa Wanawake ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kusaka maji usiku na mchana.

"Tunaishukuru Serikali kutupatia mradi huu wa maji, hatupati tena shida kama awali. Tunaomba miradi hii idumu na tuzidi kuboreshewa huduma zaidi." Alisema Bi Zuhura Mohammed Kwambika mkazi wa kijiji cha Mwenge B kilichopo kata ya Kitama.

Katika ziara hiyo ya Gavana Shilatu aliambatana na Maafisa maendeleo kata, Watendaji vijiji pamoja na uongozi wa kamati husika za maji ambapo alitembelea miradi ya maji iliyopo kata ya Kitama na kata ya Mihambwe ambayo inahudumia zaidi ya vijiji 13.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com