METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 25, 2020

Sheikh wa Mkoa wa Rukwa akanusha uzushi unaoenea mitandaoni wenye lengo la kumchafua


Shekh wa Mkoa wa Rukwa Rashid Akilimali akionyesha barua inayosambaa kwenye mitandao inayodaiwa kulenga kuchafua na kumdhalilisha.

Sheikh wa mkoa wa Rukwa Rashid Akilimali amekanusha uzushi unaoendelea kusambazwa katika mitandao ya kijamii ukimuhusisha kuandika barua ya pongezi kwenda makao makuu ya Baraza la Waislamu Tazania (BAKWATA) kwa jitihada za hali na mali zilizofanywa na Baraza hilo kuhakikisha waislamu waliogombea nafasi za uwakilishi wanashinda katika kura za maoni na hatimae kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sheikh Akilimali alisema kuwa dhamira ya barua hiyo ni kuchafua na kumdhalilisha na kuthibitisha kuwa yeye si muumini wa chama chochote cha siasa isipokuwa kazi yake tangu kampeni za uchaguzi mkuu zianze ni kuhamasisha Amani pamoja na kuwahubiria waumini kushiriki katika kupiga kura tarehe 28.10.2020 na kumchagua mtu ambaye wanamuona atawaletea maendeleo katika jimbo lao nchi yao, na mkoa wao kwa ujumla.


“Hivyo basi napenda kuwathibitiesheni kwamba barua hii, sikuiandika mimi, haina saini yangu na wala haina hata nembo ya baraza kuu la waislamu wa Tanzania, barua ambazo zinaandikwa na ofisi yet umara nyingi zinakuwa na nembo yetu, zinakuwa na kumbukumbu namba na lazima zisainiwe na mtu aliyoiandika, tunatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa waelewe barua hii ni ya kumchafua Sheikh Rashid Akilimali, barua iliyojaa ulaghai na uwongo mkubwa na si kweli yaliyotamkwa ndani ya barua hii,” Alisisitiza.


“Kama ni kuandika barua ningemu-address bosi wangu ambaye ni Mufti wa Tanzania ndio ningempelekea barua, lakini barua haioneshi hivyo, inaonesha inatoka ofisi ya mkoa inaelekea baraza kuu la Waislamu Tanzania, yaani hata mwandishi mwenyewe hana maana na wala sio mtambuzi wa mambo na amejaribu kunukuu aya za Qur’an ndani yake, aya zinazoleta mauaji na kidha wa kadha, vita huu ni uchochezi ambao mimi binafsi na baraza langu la mashekhe mkoa wa Rukwa hatulikubali,”


“Hivyo basi namtaka aliyoandika barua hii anitake radhi kabla sijamchukulia hatua za kisheria na tayari nimekwishamtambua, ofisi yangu imeshafanya uchunguzi, tumemtambua mwandishi wa barua hii, na baadhi ya wanasiasa wanaitumia barua hii kuinadi kwaajili ya maslahi yao,” Alisema.


Katika kusisitiza hilo Sheikh Akilimali ametoa siku 14 kwa mtu huyo kumuomba radhi na kuwaonya wanasiasa wote ambao wanaendelea kuinadi barua hiyo kwenye majukwaa yao ya kisiasa kuacha mara moja kwani wasipofanya hivyo atawachukulia hatua za kisheria.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com