METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 6, 2020

MAJALIWA: TUNATAKA KIONGOZI ATAKAYEPAMBANA NA RUSHWA

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kirongwe, wilayani Mafya, katika mkutano wa kampeni, Septemba 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mafya, Omar Juma Kipanga, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika Kata ya Kirongwe, wilayani Mafya, kwenye mkutano wa kampeni, Septemba 6, 2020. Katikati ni Mgombea Udiwani Kata ya Kirongwe, Said Msabah. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Mkazi wa Kata ya Kirongwe, Obed Limbu, akisoma Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, mbele ya  Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika Kata ya Kirongwe, wilayani Mafya, Septemba 6, 2020.


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kuwa na kiongozi anayeweza kuunda Serikali na mwenye uwezo wa kupambana na rushwa na mafisadi ambao wanasababisha nchi kukosa maendeleo.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kiongozi huyo ni lazima awe na uwezo wa kuisimamia Serikali atakayoiunda pamoja na kuhakikisha wateule wake wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwafuata wananchi waioshio vijijini na kuwatumikia.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 6, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kirongwe wilayani Mafia, Pwani katika mkutano wa kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Mafia,+ Omari Kipanga na wagombea wa udiwani wa CCM.


Amesema hiki ni kipindi  muafaka kwa wananchi kuhakikisha ifikapo Oktoba 28 mwaka huu wanajitokeza kwa wingi kwenda kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo na wasichague viongozi kwa ushabiki ili wasije kujilaumu mwishoni.


Mheshimiwa Majaliwa amesema kiongozi anayetakiwa katika nchi hii ni yule ambaye kwa dhamira yake anamtanguliza Mwenyezi Mungu mbele jambo ambalo litamjengea heshima katika jamii. “Lazima tupate kiongozi mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu.”


“Suala la kuimarisha amani na utulivu ni muhimu sana kwetu, tukipata kiongozi mwenye kuanzisha mtafaruku kwa kauli zake, lugha zake na matendo yake wanaoumia ni akina mama na watoto. Tuchague chama chenye uwezo na muelekeo wa kuimarisha amani”


Amesema Serikali ya CCM imejipanga vizuri kuwatumikia na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imefanya mambo mengi na aliyewafikisha hapo ni Dkt. John Magufuli ambaye leo namuombea ridhaa ya miaka mitano mingine ili akamilishe kazi aliyoianza.

Akizungumzia  suala la usafiri katika kisiwa cha Mafia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali yao imejipanga kuhakikisha inaboresha huduma hiyo na sasa inaendelea na ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia-Nyamisati. 

Amesema ujenzi wa kivuko hicho ni utekelezaji wa Ilani ya CCM Ibara ya 57 (J)) na kinajengwa kwa gharama ya sh. bilioni 5.3. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 95 na tayari kiasi cha sh. bilioni 4.1 kimetumika. Kivuko kinatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Novemba, 2020. 

Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wakazi wa Mafia uwepo wa usafiri kwa muda wote na tayari  Serikali imepeleka kivuko kingine kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati baada ya kivuko cha awali kuwa kwenye matengenezo. 

Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Nyamisati pamoja ujenzi wa gati katika badari ya Mafia ili kuboresha huduma ya usafiri wa kutoka na kuingia Mafia ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM Ibara 58(c). 

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kujenga barabara za lami nchini zikiwemo na za wilaya ya Mafia na ilianza kwa kujenga barabara zinazounganisha mikoa  na sasa inajenga barabara zinazounganisha  wilaya. 

Amesema kuwa barabara ya kutoka Kilindoni – RAS Mkumba – Mafia yenye urefu wa kilomita 55 inajengwa lengo likiwa ni kurahisisha shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo. Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Ilani ya CCM imeelekeza ununuzi wa vivuko viwili vitakavyotoa huduma kati ya Nyamisati na Mafia, hivyo baada ya kukamilika kwa kivuko cha sasa katika kipindi cha miaka mitano kitajengwa kivuko kingine ili kuondoa changamoto ya usafiri katika maeneo hayo.

 

Akizungumzia kuhusu masuala ya uvuvi, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuimarisha ulinzi kwa wavuvi Serikali itanunua boti saba  zitakazotumika ili kuimarisha doria ambapo wilaya ya Mafia itapewa boti pamoja na kuongezewa askari wa doria.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com