Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi kwenye eneo la
machimbo ya dhahabu la Kwandege lililopo wilayani Handeni mkoani Tanga tarehe
25 Juni, 2020.
Wananchi
wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (hayupo pichani) kwenye eneo la machimbo ya dhahabu la Kwandege lililopo
wilayani Handeni mkoani Tanga tarehe 25 Juni, 2020.
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametatua
mgogoro wa muda mrefu kati ya mmliki wa machimbo ya dhahabu ya Kwandege
yaliyopo wilayani Handeni mkoani Tanga,
Godfrey Bitesigirwe na wananchi wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini
katika machimbo hayo mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu
ya ziara yake mkoani Tanga yenye lengo
la kukagua shughuli za madini na kutatua changamoto mbalimbali.
Mara baada
ya kusikiliza kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi kupitia mkutano wa
hadhara mapema jana tarehe 25 Juni, 2020 alielekeza mmiliki wa leseni ya
madini, Godfrey Bitesigirwe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu
Napacho, Afisa Mgodi Mkazi wa Handeni na wananchi kukaa pamoja na kuweka
makubaliano ya pamoja yatakayowezesha wananchi na mmiliki wa leseni kunufaika kwa
pamoja huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Aidha Naibu
Waziri Nyongo alielekeza kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho kwa mkataba
kati ya wachimbaji wa madini na mmiliki wa leseni ili kuondoa kasoro zilizokuwa
zinalalamikiwa na wananchi hao.
Alisema
kuwa ili kuhakikisha wananchi maskini wananufaika na rasilimali za madini, Serikali imeweka
utaratibu wa kurasimisha wachimbaji wasio rasmi na kuwasaidia ili waweze
kutajirika huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.
Katika
hatua nyingine Nyongo aliwataka wananchi kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni
za madini huku wakijikinga na magonjwa hatarishi kama COVID 19.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alimpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Tanga, Zabibu Napacho na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe kwa hatua za
awali za utatuzi wa mgogoro zilizofanywa kwa mafanikio makubwa.
Awali
akisimulia historia ya mgogoro huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu
Napacho alieleza kuwa awali ofisi yake ilipata taarifa za kuwepo kwa uvamizi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika
eneo la kijiji cha Kwandege kwenye
leseni inayomilikiwa na Godfrey Bitesigirwe ambapo ofisi ilimshauri kuchukua hatua za kuzuia uchimbaji usio rasmi
ili kuepusha ajali pamoja na upotevu wa kodi za serikali pamoja na utoroshaji
wa madini.
Alisema
kuwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Ofisi ya
Afisa Migodi Mkazi wa Handeni na Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya
Handeni ilifanya ukaguzi ili kujionea hali halisi na kubaini wachimbaji 300
wakiendelea na shughuli za uchimbaji kwenye leseni husika na kuwataka
wachimbaji hao kusubiri utaratibu maalum utakaowekwa kabla ya kuendelea na
shughuli za uchimbaji.
Aliendelea
kusema kuwa katika hatua nyingine, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga
iliwaelekeza wamiliki wa ardhi katika maeneo yenye leseni za uchimbaji wa
madini kukutana na mmiliki wa leseni ambapo mara baada ya kukutana
walikubaliana wamiliki wa mashamba katika maeneo yatakayofanyika uchimbaji wa
madini ya dhahabu kupata asilimia saba ya thamani ya madini baada ya tozo za
Serikali na gharama zote za uchimbaji wa madini
kuwa chini ya mmiliki wa leseni.
Makubaliano
mengine yalikuwa ni pamoja na umiliki wa mashamba kuendelea kuwa chini ya
wamiliki na tozo za Serikali ambazo ni
mrabaha asilimia 6 ada ya ukaguzi asilimia 1 na ushuru wa huduma za jamii 0.3
ya thamani ya madini zitakatwa kabla ya mgawanyo wa makubaliano.
Awali
wakizungumza kwa nyakati tofauti mbali na kuipongeza Wizara ya Madini kwa
kumaliza mgogoro wananchi hao walieleza
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutozwa kodi ambazo zingetakiwa
kulipwa na mmiliki wa leseni ya madini na ukosefu wa vifaa vya uchimbaji wa
madini.
0 comments:
Post a Comment