METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 22, 2020

LETENI MBUNGE WA KUPITISHA BAJETI, SIYO WA KUPINGA TU - MAJALIWA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni  kwenye uwanja wa Ukote, Kilwa Kivinje, Oktoba 22, 2020.

Baadhi ya wananchi wa Kilwa wakimshangilia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ukote, Kilwa Kiviunje Oktoba 22, 2020
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akimnadi Mgombea Ubunge wa CCM wa Jimbo la Kilwa Kusini, Ali Mohammed Kasinge (kulia) na Mgombea Udiwani wa Kata ya  Kivinje Singino, Jafar Arobaini katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye uwanja wa Ukote, Kilwa Kivinje mkoani Lindi, Oktoba 22, 2020.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Kilwa wamchague mbunge ambaye atakuwa tayari kupitisha bajeti na kuwaletea maendeleo.

 

“Msilete watu wa kukataa fedha, bali leteni mtu wa kukubali fedha zipitishwe ili mpate maendeleo,” amesema.


Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba 22, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Ilulu Njianne katika kata ya Tingi na kata ya Kivinje kwenye mikutano iliyofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi.

 

“Tanzania inahitaji watu makini na pale Bungeni siyo mahali pa viburudisho. Bunge linahitaji watu wa kuwasemea wananchi na siyo kuleta burudani wakati wengine wako kazini,” amesema.

 

Mheshimiwa Majaliwa leo yuko mkoani Lindi kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Ametumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge wa majimbo ya Kilwa Kaskazini, Bw. Francis Ndulane na Kilwa Kusini, Bw. Ally Kasinge pamoja na wagombea udiwani wa kata za majimbo hayo kwa tiketi ya CCM.

 

“Mleteni mtu anayeweza kujenga hoja na kuitetea. Fedha zisipopitishwa maendeleo yenu hayawezi kuja kwa sababu hakuna mtu wa kuwasemea. Wana-Kilwa msiniangushe, Jumatano ijayo ikifika, chukua karatasi yako weka tiki kwa Dkt. Magufuli; kwa mbunge wa CCM na kwa diwani wa CCM.”

 

Aliwataka wakazi hao wawachague wagombea wa CCM kwa sababu chama hicho kina makada wazuri na kimewaandaa vizuri viongozi wake. “Kitendo cha Kamati Kuu kuwapa nafasi hawa waliopitishwa, hakikuwa na nia ya kumuonea mtu bali kuwapanga viongozi wake kulingana na majukumu.”

 

Mapema, mtia nia aliyeongoza kwenye kura za maoni katika jimbo la Kilwa Kaskazini, Bw. Murtaza Mangungu alipopewa nafasi ya kuwaombea kura wagombea wa CCM alitumia fursa hiyo kuwaonya watu wanaoweka maneno maneno dhidi yake.

 

“Wako watu ambao walitaka kusafiria nyota yangu. Wakati tunazindua kampeni, nilitamka kutoka moyoni mwangu, siyo kinywani tu, kwamba nitafanya kazi kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinashinda. Namuombea kura Dkt. Magufuli, namuombea kura kaka yangu Francis Ndulane na mgombea udiwani wa Tingi, Rajab Ngatanda,” alisema.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com