METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, September 22, 2020

WADAU WA MADINI WASHAURIWA KUUNGANA ILI KUZALISHA KWA TIJA

Waziri wa Madini Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni katika banda la wizara ya madini alipotembelea Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Septemba 21, 2020 mkoani Geita.

Waziri Biteko akisaini  kitabu cha wageni katika banda la benki ya CRDB alipotembelea Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Septemba 21, 2020 mkoani Geita.

Waziri wa Madini Doto Biteko amewashauri Wadau wa Madini wa Mkoa wa Geita kuungana na kutengeneza Kampuni ya pamoja ili kuongeza tija katika shughuli zao. 

Ushauri huo, ameutoa mara baada ya kutembelea Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita. 

Wakati huo huo, Waziri Biteko ametoa pongezi kwa waandaji wa Maonesho hayo ambayo mwaka huu zaidi ya kampuni 420 zinashiriki. 

Vilevile, Waziri Biteko ametoa Wito kwa taasisi za Kibenki kuendelea kuwalea Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara ya Madini kwa kuwapa mafunzo pamoja na mikopo ili wazalishe kwa faida. 

Naye, Mkurugenzi wa Mikopo kwa Wajasiliamali Wadogo wa NBC Elibariki Masuke, amesema Benki ya NBC Mkoa wa Geita imetoa mkopo wa zaidi ya Shilingi bilioni 4.4 kwa Wadau wa Sekta ya Madini mkoani humo ili kuwaongezea uwezo katika shughuli zao. 

Hayo aliyasema mbele ya Waziri Biteko alipotembelea banda la la benki ya NBC katika Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita. 

Imeelezwa kuwa, wanufaika wa mikopo hiyo ni pamoja na Wachimbaji Wadogo, Wafanyabiashara ya Madini na Wachenjuaji wa Madini wa Mkoa wa Geita. 

"Sisi kama Benki ya NBC tumeanza kutoa mafunzo kwa Wadau wa Madini hususan Wachimbaji Wadogo wa dhahabu na Wafanyabiashara ya dhahabu ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwekeza katika Sekta ya Madini", alisema Masuke. 

Pamoja na mambo mengine, Masuke amesema Banki ya NBC imekuwa Mdau Mkubwa kwenye Sekta ya Madini  ambapo mpaka sasa kuna taratibu zinawekwa sawa ili mikopo mikubwa zaidi ianze kutolewa kwa Wadau wa Sekta ya Madini kote nchini.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com