Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kipande Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Morogoro hadi Mkakutupora Singida Mhandisi Mteshi Tito wakati wa ziara yao ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na Serikali nchini.

Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo wakishuka katika treni ya kisasa inayotumia umeme katika kituo cha Soga
mkoani Pwani wakati wa ziara yao ya kutembelea mradi wa Reli ya Kisasa (SGR)
unaotekelezwa na Serikali nchini.
Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
wakipata maelezo kabla ya kupanda treni ya majaribio inayotumia umeme wakati wa
ziara yao ya kutembelea mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotekelezwa na Serikali
nchini.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotekelezwa
na Serikali nchini utawanufaisha watanzania wote moja kwa moja ikiwa ni ajira
kwa upande wa reli yenyewe, kilimo, ama biashara hatua inayosaidia kuinua
kipato na uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa hatua ya awali mradi unamanufaa makubwa
na umetoa ajira kwa Watanzania asilimia
51 na wageni asilimia 49 tofauti na hapo awali ambapo ilipangwa wataalamu wa
ndani wawe asilimia 20 na wataalamu wan je ya nchi wawe asilimia 80.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Kipande cha
Morogoro Mkakutupora Singida Mhandisi Mteshi Tito kwa wajumbe wa Menejimenti ya
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati wa siku ya pili ya ziara
yao ya kutembe mradi huo na kuongeza hatua hiyo ya uwiano huo wa ajira
imefikiwa baada ya Watanzania kuonesha uwezo mkubwa wa uelewa kwenye masuala ya
reli.
Aidha, mradi huo unaendelea kutoa ajira kwa
watanzania katika maeneo yao ambapo unapita ikizingatiwa ni mradi mkubwa
unaopitia mikoa mingi inapopita reli kuanzia Dar es salaam, Pwani, Morogoro,
Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kigoma ambapo unatarajiwa kufika.
Fauka ya hayo mradi pia unatarajiwa kuwa
kutoa fursa nyingi za kiuchumi ambapo utasaidia kusafirisha mizigo kwenda nchi
jirani zisizo na bandari ikiwemo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasiaya
Kongo na Uganda hatua itakayosaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa nchi.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Jamila Mbaruku amewapongeza wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na moyo wa uzalendo wa kuthamini na
kuchukua hatua ya kujionea mradi unaotekelezwa na Serikali kwa fedha za ndani.
“Naamini mtakuwa mabalozi na wajumbe wazuri
kwa kuwatangazia Watanzania juu ya mradi wetu huu wa reli ya SGR kwa kuwa ninyi
ndiyo wizara yenye kuisemea Serikali, mmeuthamini, mmethubutu na mmeweza
kutembelea eneo lote inapopita reli yetu kutoka kituo cha Ihumwa Dodoma hadi
kituo kikuu eneo la Posta jijini Dar es Salaam” alisema Jamila.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Utawala
na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Zahara Nguga amesema kuwa kuna dhana potofu
inayoenezwa na watu kuwa mradi huo utawanufaisha wafanyakazi peke yao, la
hasha, mradi huo utawanufaisha pia wafanyabiashara na wakulima kutoka maeneo
mbalimbali inapopita reli hiyo.
“Hata wakulima, mtu anaweze kuwekeza Kilosa
akatoka Dar es salaam saa 11 asubuhi na saa 1 yupo Kilosa akisimamia mifugo,
mashamba na mazao yake na jioni anarudi Dar es Salaam kuimarisha maisha yake ya
ndoa. Huu ni mradi unawanufaisha watanzania wote” alisisitiza Mkurugenzi
Msaidizi huyo.
Wakitoa neno la shukrani kwa niaba ya
Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo, Mkuu wa Idara ya Sera na Mipango Petro
Lyatuu pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Leah Kihimbi
wamesema kuwa waliazimia kutembelea mradi huo kwa kuzingatia wizara yao ndiyo
yenye dhamana ya habari na mradi huo hauna budi kutangazwa na vyombo vya habari
ili kuwaelimisha na kuwapa uelewa wananchi juu ya miradi inayotekelezwa na nchi
yao.
Lengo la ziara yao la kuufahamu mradi huo
limefikiwa kwa kuwa wamejionea malighafi zinazotumika kuutekeleza zinatoka hapa
nchini ikiwemo saruji na nondo
zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania na baada ya kukamilika utakuwa na
manufaa mengi ikiwemo matumizi mazuri ya muda wa kusafiri ambapo muda wa
kusafiri kutoka Dodoma hadi Dar es
salaam utakuwa ni saa tatu na Morogoro hadi Dar es Salaam itakuwa ni dakika 90
sawa na saa 1:30.
Aidha, wameongeza kuwa wamepanda treni inayotumia umeme inayotumiwa na wahandisi kutekeleza majukumu yao na kusema ukiwa ndani ya treni hiyo unaweza kuendelea kufanya kazi za ofisini bila kuwa na mtikisiko wowote na kuongeza kuwa mradi umekuja umejali maisha ya watu kwa maana watautumia na Shirika la Reli limejali vitu vya asili vya kuitamaduni ikiwemo mito na miti ambayo wameitunza vizuri.
0 comments:
Post a Comment