METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 26, 2020

DKT.KALEMANI AZINDUA REA KITONGOJI KWA KITONGOJI

Wananchi wa Kitongoji  cha Migombani,Kijiji cha Bukene, Wilaya ya Nzega, Mkoani wa Tabora, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani,(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mradi 

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani(mwenye shati la bluu) akikata utepe kuashiria kwa uzinduzi wa usambazaji umeme katika kila kitongoji nchini uliofanyika katika kitongoji cha migombani,kijiji cha Bukene, wilaya ya Nzega, Mkoani wa Tabora,Septemba 24,2020,(kulia) Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt.Philemon Sengati(kushoto) Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati vijiji(REA) Wakili Julius Kalolo.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amezindua rasmi usambazaji wa Umeme katika kila kitongoji nchini ambapo jumla ya vitongoji 64,839 nchini kote vinatarajiwa kuungalishwa na umeme kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa.

Uzinduzi rasmi wa usambazaji umeme katika kila Kitongoji umefanyika katika Kitongoji cha Ufuruma Kijiji cha Ufuruma Wilayani Uyui na katika Kitongoji cha Migombani Kijiji cha Bukene Wilayani Nzega mkoani Tabora, Septemba 24, 2020.

Dkt. Kalemani alisema kuwa mradi huo utagharimu fedha za kitanzania shilingi Bilioni 297.7 na kwamba mradi huo ni endelevu.

Akizungumzia sababu ya kuchagua Mkoa wa Tabora kuwa kitovu cha kuzindua mradi huo, Dkt. Kalemani alisema kuwa mkoa huo ni mkubwa ikilinganishwa na mikoa mingine nchini, pia una idadi kubwa ya vitongoji ambavyo bado havijaunganishwa kabisa na umeme.

Katika mkoa huo, Vitongoji 122 vinatajiwa kuunganishiwa umeme na Kampuni ya Ukandarasi ya Sengerema ambayo ndiyo imepewa dhamana ya kutekeleza kazi hiyo katika vijiji hivyo ambapo ameahidi kutekeleza mradi huo ndani ya kipindi cha miezi Tisa, badala ya Miezi 12.

“Naomba tuelewane watanzania, Rais Magufuli na Serikali yake alikwisha toa fedha za kupeleka umeme kwenye vijiji vyote na vitongoji vyote,niwaombe watanzania kwenye masuala ya umeme tulieni umeme unakuja kila kitongoji bila kujali kwamba kimeguswa au laa, sasa ni rasmi kuwa vitongoji vyote vinaletewa umeme ,mnachotakiwa wananchi ni kusuka nyaya katika nyumba zenu na umeme huu haubagui nyumba,” alisisitiza Dkt. Kalemani. 

Aidha aliendelea kuwataka wananchi kuendelea kulipia gharama za kuunganishiwa umeme bila kusubiri nguzo kuwafikia kwa kuwa tayari umeme utafika katika kila kitongoji kwa gharama ya shilingi 27,000 tu. 

Vilevile alisema kuwa wananchi hawapaswi kuhoji kuhusu nguzo kufika katika maeneo yao kwakuwa hilo si jukumu lao, wanachotakiwa kufanya ni kulipia gharama za kuwashiwa umeme tu, na baada ya kulipia gharama ndipo wahoji endapo hawajawashiwa umeme. 

Aliwata REA na TANESCO kushirikiana na serikali za vijiji, wilaya na mikoa kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa umeme na kuunganishwa. 

Hata hivyo aliwaonya baadhi ya wakandarasi wenye tabia ya kuruka nyumba za wateja kuwa hiyo haitakubalika na yeyote atakaye binika kufanya hivyo hatua za kisheria itachukuliwa dhidi yake. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa huo, Dkt. Philemon Sengati aliwaasa wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya umeme kwa kuanzisha viwanda vidogo ili kuinua uchumi wao na taifa kwa jumla.

Aidha amewataka kutunza miundombinu ya mradi huo na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaoetekeleza mradi huo na kwamba vijana watakaopata ajira wawe wazalendo na kuzingatia kuwa miradi hiyo ni kwa ajili ya watanzania.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com