METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 26, 2020

BILIONI 276 KUMALIZA ADHA YA MAJI ILEMELA

Zaidi ya shilingi bilioni 276 inategemewa kumaliza adha na kero ya maji ndani ya jimbo la Ilemela na majimbo jirani yakiwemo Nyamagana na Magu.

Hayo yamesemwa na mgombea ubunge jimbo la Ilemela kupitia chama cha mapinduzi Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na maelfu ya wananchi na wanachama wa chama hicho waliojitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Kangae 'A' kata ya Nyakato ambapo amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli imetoa fedha hizo kwaajili ya kutatua kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza hususani jimbo la Ilemela 

' Dkt Magufuli amewekeza zaidi ya bilioni 276 kumaliza kero ya maji kwa Ilemela na majirani zake wa Nyamagana na Magu ' Alisema

Aidha Dkt Mabula ameongeza kuwa wakati anaingia madarakani mwaka 2015 jimbo la Ilemela kupitia manispaa lilikuwa na uwezo wa kukopesha jumla ya shilingi milioni 216 na mpaka mwaka huu 2020 wamefanikiwa kuongeza fedha za mikopo kwa Vijana, wakina mama NA watu wenye ulemavu kufika shilingi bilioni 1 na milioni 431 huku sheria ikitungwa kwaajili ya kusimamia utoaji wa fedha hizo tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mikopo hiyo ilikuwa ikitolewa kwa utashi wa watu wachache kupelekea baadhi ya watu kutonufaika nayo.

Akimkaribisha mgombea huyo, Meneja kampeni Ndugu Kazungu Safari Idebe akasema kuwa zipo sababu zaidi ya milioni juu ya kwanini wananchi hao wakichague chama cha mapinduzi na wagombea wake ikiwemo ujenzi wa miradi ya kimkakati ya upanuzi wa uwanja wa ndege, ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa meli na vivuko ndani ya ziwa Victoria na maziwa mengine, ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa na mradi wa ufuaji wa umeme wa Mwalimu Nyerere.

Nae mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Ilemela Ndugu Nelson Mesha akawaomba wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kukiamini tena chama chake na kuwachagua Dkt John Magufuli kwa nafasi ya Urais, Dkt Angeline Mabula kwa nafasi ya ubunge huku nafasi ya udiwani akiomba wapewe madiwani wote wanaogombea kwa tiketi ya chama hicho.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com