Prof Esnat Chaggu Mwenyekiti wa Bodi – Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC akisisitiza jambo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi wa Mazingira katika Wilaya ya Songwe hii leo.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima ameuagiza
uongozi wa Wilaya ya Songwe kuwabaini, kuwasajili na kuunda vikundi vya
wachimbaji wadogo wasio rasmi ili waweze kutambulika na kufaidika na mikopo
midogo midogo inayotolewa na Serikali hapa nchini.
Ameyasema
hayo hii leo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe
hususan Wilaya ya Songwe na kubaini changamoto ya wachimbaji wadogo wanaoharibu
mazingira kutokana na uchimbaji holela.
“Ni lazima
mchukue hatua za haraka za kuwatambua wachimbaji hawa kwa lengo la kuwasajili
na kuanzisha kanzi data itakayosaidia katika zoezi la utoaji wa elimu ili
kunusuru mazingira” Sima alisisitiza.
Waziri Sima
amesisitiza kuwa ni vema pia Wilaya ya Songwe ikaanzisha vikundi vya mazingira
na kuhamasisha matumizi ya Sheria ndogondogo katika maeneo yao.
Akiwasilisha
taarifa ya hali ya Mazingira katika Wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya ya Samuel
Jeremia Opulukwa amesema Wilaya yake inakabiliwa na changamoto kubwa za
uchomaji wa misitu unaohatarisha maisha ya viumbe hai na ikolojia ya eneo hilo.
Katika
hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ametoa wito kwa watafiti wa madini katika
eneo hilo kutoa taarifa rasmi katika ngazi ya Wilaya ili kuepuka uharibifu wa
mazingira unaofanywa na watafiti hao kwa kuchimba kiholela kwa lengo la
kutafuta dhahabu.
Pia, Naibu
Waziri Sima ametembelea Mgodi wa Shanta na kuagiza uongozi wa mgodi huo kutoa
elimu kwa jamii inayozunguka mgodi huo juu ya namna bora ya uchimbaji wa madini
kwa njia bora na salama kwa mazingira.
“Kwa kuwa
mgodi huu unatumia teknolojia ya kisasa zaidi, natoa rai kwa mgodi kuhamisha
teknolojia hii kwa wachimbaji wadogo wadogo ili wananchi pia wanufaike” Sima
alisisitiza.
Mheshimiwa Mussa Sima yuko Mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi na ametembelea Wilaya ya Songwe na kukagua usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ambapo kesho atawasili Mkoani Mbeya.
0 comments:
Post a Comment