METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 21, 2020

SI MUDA WA KULALAMIKA, TUJITAFAKARI, TUJIREKEBISHE NA KUONYESHA UKOMAVU WA KISIASA- PATRICK MYOVELA


Anaandika Patrick Myovela, Mwandishi wa vitabu Tanzania

Kwa muda wa miezi miwili sasa, joto na presha kwa wanasiasa wengi nchini Tanzania vilikuwa katika vipimo tofauti  vyenye kuonyesha kupanda na kushuka kwa nyakati zote bila kufuata mpango maalumu unaoratibiwa na miili yao.

Hali hii ilikuwa ngumu zaidi kwa wanasiasa waliotia nia kupitia Chama cha Mapinduzi kwasababu mbali na upinzani waliokuwa wakipeana wao kwa wao ndani ya chama, zaidi walitakiwa kujikita katika kufuata miiko ya chama ya kuwa waadilifu katika kuzipigania nafasi walizokuwa wakizigombea.

Ili kuthibitisha hilo kwa nyakati tofauti tofauti Chama cha Mapinduzi kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa  Dr Magufuli, Katibu Mkuu Dr Bashiru na hata kwa katibu mwenezi wake wa Chama ndugu  Polepole wamekuwa mstari wa mbele kuwakumbusha wagombea wote kwa nafasi zote kuzingatia uadilifu wakati wote wa kabla na hata baada ya kura za maoni  ndani ya Chama cha Mapinduzi.

Ni ukweli usiofichika kwani wapo waliokwenda kinyume na kujikuta wakitumbukia kwenye karai la kutokuzingatia neno uadilifu lililokuwa likipigiwa chapuo na viongozi wakuu wa Chama na kuona wanaweza kufanya kinyume na ushauri wao na wakafanikiwa katika mbio za ama kupata nafasi walizogombea au kuzitetea nafasi zao za awali. 

Mdudu Rushwa akawapanda kichwani na kujifanyia waliyoona kwao ni sahihi huku wakisahau neno uadilifu vichwani mwao.

Jana tarehe 20.08.2020 kupitia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Chama cha Mapinduzi kilifanya uamuzi wake wa mwisho na kuteua majina ya  wagombea Ubunge watakao peperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Nina uhakika CCM imefanya uamuzi huo baada ya kujitosheleza na taarifa inazozipata kupitia vyombo vyake vya Usalama na Maadili ya Chama, Kamati za siasa za kata, Wilaya na Mkoa, TAKUKURU  na kadhalika. 

Uamuzi uliofanyika jana na Chama cha Mapinduzi ni katika kuzingatia moja ya malengo ya chama chochote kile cha siasa yanayokitaka chama kushika dola. Naamini katika hili kimejipanga  kisawasawa mpaka kufikia uamuzi wa mwisho kwa siku ya  jana.

Baada ya uamuzi wa chama cha Mapinduzi kupitia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa jana, bila shaka wagombea, wanachama na watanzania kwa ujumla wamekuwa na maswali ya kwanini fulani hajarudi na kwanini fulani karudi. 

Hii si mara ya kwanza kwa chama kufanya maamuzi kama haya. Kwani hata miaka ya nyuma katika baadhi ya majimbo, teuzi zenye sura ya mabadiliko zilifanyika pia. Na zaidi kwa kuzingatia taarifa toshelevu za vyombo vya chama cha Mapinduzi vinavyowajibika kuhakikisha kuwa  chama kinapata taarifa sahihi.

Muda si mrefu kipenga cha kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu kitalia katika hili niwasihi wana CCM wenzangu kuacha kulalamika kwasasa mchakato uliopita uwe ni moja ya nyenzo ya kusaidia kujifanyia tathmini ya maisha na mwenendo wa kisiasa kwa ujumla. Lazima mtambue kuwa kama haijawezekana leo basi itakuwa kesho, lakini kama tutazingatia zaidi kuishi katika miiko na misingi ya chama chetu. 

Muda huu ni wa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na kuachana na hasira za mkizi kwani  wapo wengi watakaowashauri  kuhama chama kwa maneno matamu ya kuwataka kuwa huru na zaidi kwa kusema mtatekeleza misingi ya demokrasia wakidhani wanawasaidia kumbe sivyo.

Tunzeni heshima yenu kwa busara ya kukubali kuwa katika mashindano yoyote lazima mshindi apatikane. Zaidi ningewasihi myakumbuke maneno ya ndugu yetu Rais mstaafu Dr Jakaya Kikwete yasemayo " *Akili za kuambiwa changanya na za kwako* " .Msikurupuke kufanya maamuzi yasiyo na afya hata mara moja kwa ustawi wa maisha yenu kisiasa kwani mifano mnayo yakutosha mpaka sasa kwa waliothubutu kufanya hivyo. 

Katika hili niwawakumbushe pia wale wote waliokuwa wakimuunga mkono mgombea fulani aliyeongoza katika kura za maoni na kukosa uteuzi wa mwisho kutokuwa sehemu na chachu ya kumtia jeuri na kiburi mgombea huyo,akajiona yeye ni bora ama zaidi ya chama . Lazima kama wanachama wakumbuke kuwa chama cha Mapinduzi ni zaidi ya mgombea. Niwasihi kutumia busara ya kuhimizana kuwa kitu kimoja katika kukipigania chama na kukiletea ushindi. 

Kwa wote mliopewa dhamana na chama ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu msijisifu kuwa ninyi ni bora kuliko wengine. Kaweni wasikivu na watendaji. Kavunjeni makundi yaliyokuwepo kupindi cha mchakato wa kura za maoni na kuwa kitu kimoja. Katika hili ni lazima kutumia busara kubwa ya kuhakikisha wanachama wote wanakuwa kitu kimoja na kusahau tofauti zenu zilizoibuka ndani ya muda mfupi. 

Nirudie kusema kwa wote walioshindwa na kupitishwa na chama kuwa  KULALAMIKA SI SILAHA TENA KWA SASA...KUBWA TUJITATHMINI NA KUONYESHA UKOMAVU  WA KISIASA KWA  KUKIPIGANIA CHAMA CHETU  ILI KISHINDE KATIKA UCHAGUZI MKUU KWA NAFASI YA URAIS, UBUNGE NA MADIWANI.

 *_MUNGU hutoa riziki kwa foleni, hata kama ni ndefu, zamu yako siku moja  itafika.*__ 

Patrick Myovela 

Mwandishi wa vitabu Tanzania. 

0765475941

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com