METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 7, 2021

TUMEAMUA KUREJESHA HADHI NA HESHIMA YA USHIRIKA NCHINI – WAZIRI WA KILIMO PROF. MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiwahutubia Warajis Wasaidizi wa mikoa ya Tanzania Bara Januari 6, 2021 katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi yakiwemo magari pamoja na kompyuta katika Ofisi za Tume ya Maendeleo ya Ushirika Jijini Dodoma.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akimkabidhi Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Simiyu Bwana Ibrahim Kadudu gari aina ya Nissan Hard N 300 Double Cabin 4WD Januari 6,2021 katika Ofisi za Tume ya Maendeleo ya Ushirika Jijini Dodoma.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kurudisha heshina na hadhi ya Ushirika na ndiyo maana hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa ikiwemo ya kurejesha mali za Ushirika zilizoporwa zenye thamani ya zaidi ya Bilioni 61.

Waziri wa Kilimo Prof. Mkenda ameyasema hayo Januari 6, 2021 wakati akiwakabidhi Warajis Wasaidizi magali mapya manne yenye tahamani ya shilingi milioni 275 katika Ofisi za Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Jijini Dodoma.

Waziri Mkenda amesema kabla Tazania haijapata uhuru; Tasnia ya Ushirika ilikuwa ikifanya vizuri na kutoa mfano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha mkoa wa Kilimanjaro (Kilimanjaro Cooperatives Union – KNCU) kilichokuwa kikiwaunganisha Wakulima wa zao la kahawa na kuongeza kuwa kilianzishwa mwaka 1925 na kwamba Barani Afrika Tanzania ilifanya vizuri kiasi cha nchi nyingine kuja kujifunza.

Waziri Mkenda ameongeza licha ya KNCU kufanya vizuri Shirikisho la Vyama vya Ushirika kutoka Kanda ya Ziwa (Victoria Federation) nayo ilikuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika katika miaka ya hamsini (1950s) na kuongeza kuwa juhudi zinazofanywa katika Awamu ya Tano lengo lake ni kurejesha heshima na hadhi hiyo ili kuleta mapinduzi ya kweli kwenye Sekta za Kiuchumi Sekta ya Kilimo ikiwa ni miongoni mwao.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa ili kurejesha hadhi hiyo; Wizara imeandaa mpango wa kuipitia upya Sheria ya Vyama Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 ili kuifanyia marekebisho iendane sawa na mahitaji ya sasa.

“Warajis pamoja na Washiriki wa hafla hii; Wizara imeona ipo haja ya kuipitia upya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013. Mchakato wa kuipitia utawashirikisha Wadau wote na hata wale magwiji ambao Ushirika ulifanya vizuri wakati wao, tutakutana nao na watatupa maoni yao”.

“Kupitia maoni ya Wadau ambayo yatakuwa shirikishi; Tutapata Sheria nzuri ambayo itakidhi matakwa ya wakati na ambauo itajibu changamoto kadhaa tunazokutana nazo kwa sasa”. Amekaririwa Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda amesema lengo la kufanya hivyo ili kuhakikisha Sheria mpya anajenga mazingira wezeshi ya kuipeleka Tasnia ya Ushirika kwenye maendeleo ya kweli na endelevu nchini.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa jambo lingine ambalo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kama msimamizi wa Tasnia ya Ushirika ni kuendelea kupambana na Wezi na Wabadhirifu wa mali za Wanaushirika.

“Tutaendeleo kupambana ili kuondoa wizi na ubadhirifu; Ofisi ya Waziri Mkuu imetusaidia sana kupambana na ubadhilifu. Nawaomba Warajis Wasaidizi tusaidiane kwenye jambo hilo”.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa ili kuendelea kurejesha hadhi na heshima ya Ushirika nchini Wizara itaendelea kuwajendea uwezo Wasimamizi katika Tasnia kwa kuwa huko udhibiti na usimamizi ni jukumu la muhimu kwenye maendeleo ya tasnia ya Ushirika.

“Ndugu zangu kuna haja ya kufanya maboresho makubwa kwenye utunzaji wa kumbukumbu; Kumbukumbu zisipokaa vizuri tutakuwa na changamoto kubwa kwenye usimamizi na udhibiti kwa kuwa hayo ni moja ya majukumu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika.” Amekaririwa Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa kwenye eneo la utunzanji wa kumbukumbu usioridhisha umetia doa utendaji wa Vyama vingi vya Ushirika kwenye Taarifa ya Shirikisho Ukaguzi la Vyama vya Ushirika nchini (COASCO).

Waziri Mkenda ametolea mfano Vyama Vikuu vya Ushirika 43 havijapata hati safi na ukiangalia siyo kwamba kuna wizi ila Wasimamizi hawakuwa na uwezo wa kuweka kumbukumbu vizuri

Katika taarifa ya COASCO jumla ya Vyama vya Akiba na Mikopo 3,374. Ni Vyama 34 tu ndivyo vimepata hata safi ila ukiangalia siyo Vyama vyote vya Akiba na Mikopo fedha za Wanachama vimeibwa ila ni uwekaji wa taarifa za hesabu na kubukumbu hazijawekwa vizuri.

Wakati huohuo Waziri Mkenda amevipongeza Vyama Vikuu vya Kahama (Kahama Cooperatives Union – KACU) na Chama Kikuu cha Wilaya ya Karagwe na Missenyi (Karagwe Cooperative Union – KDCU) kwa kufanya vizuri kwenye tasnia ya ushirika wa mazao, hususan zao la kahawa.

“Vyama hivi vimekuwa kielelez na sote tunapaswa kuwapongeza; Walichofanya vizuri Karagwe na Kahama. Tunapaswa tukiige kote nchini. Vyama hivi vimetupa matumaini makubwa.” Amekaririwa Waaziri Mkenda.

Aidha Waziri Mkenda amepongeza Wanachama na Uongozi wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wilaya ya Rombo (MAMSELA AMCOS) pamoja na Chama cha Ushirika wa Mpunga Bonde la Mto Ruvu (CHAURU) kwa kufanya vizuri na kuwa mfano wa kuigwa.

Aidha Waziri Mkenda amekipongeza Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Korosho wa Wilaya ya Nanyumbu, Masasi na Mtwara Cooperative Union (Nanyumbu, Masasi and Mtwara Cooperative Union - MAMCU).

“Chama Kikuu cha MAMCU kimefanya vizuri; tunatakiwa wote tujifunze kutoka kwao, wanauza mazao mapaka nje ya nchi, wanasimamia ubora za zao la korosho.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com