METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 6, 2020

VIJIJI 70 WILAYA YA IRINGA KUNUFAIKA NA UPIMAJI WA AWAMU YA PILI YA MRADI WA LTA

Kaimu Mkurugenzi wa Mradi wa LTA Mustafa Issa akiongea na washirika wa semina ya utekelezaji wa mradi huo awamu ya pili katika wilaya ya Iringa.
Afisa wa uenezi wa mradi LTA Jackline Mhegi akitoa elimu kwa wajumbe waliokuwa wanashirki warsha ya mradi wa upimaji ardhi awamu ya pili


NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

KATIKA kukabiliana na  migogoro ya ardhi katika mikoa ya Iringa na Mbeya mradi wa kurasimisha ardhi vijijini unaowezeshwa na shirika la maendeleo la kimataifa la Marekani (USAID) Land Tenure Assstance  (LTA) chini ya mpango wa feed the future imeingia katika awamu ya pili ya mradi ambapo wameendesha mafunzo  maalumu kwa watendaji wa kata na maafisa tarafa wa wilaya za mkoa wa Iringa

Akizungumza mara baada ya kutoa mafunzo ya urasimishishaji Ardhi kwa watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa ambao Mradi huo unatekelezwa katika maeneo yao, Kaimu Mkurugenzi wa Mradi wa LTA Mustafa Issa amesema kuwa lengo ni kuwezesha wanakijiji kuthamini Ardhi zao.

Issa alisema kuwa asilimia tano 5% ya michango yote ya wanakijiji itakapofikiwa na kamati ya usajili wa ardhi ya kijiji itaomba kuanza utekelezaji wa zoezi la uhakiki wa mipaka ya ardhi ya kijiji na uandaji wa cheti cha ardhi ya kijiji.

Alisema kuwa endapo wanakijiji watafikisha asilimia kumi  10% ya michango yote  kamati ya usajili wa ardhi ya kijiji itaomba kuanza kwa zoezi la maandalizi ya mpango wa matumizi bora ya ardhi na hatua za awali za uhamasishaji juu ya mafunzo ya uelewa kwa  halmasahuri za vijiji na mkutano mkuu.

Issa alisema kuwa LTA itawasilisha ripoti kamili ya utekelezaji wa shughuli na maombi ya malipo ya 100% ya michango ya wanakijiji kwa kuzingatia idadi halisi ya vipande vilivyopimwa kwa halmashauri ya kijiji, idara ya ardhi na kamati ya usajili wa ardhi ya kijiji baada ya wiki ya nne toka kuanza kwa zoezi la kudurufu na kusajili hatimiliki za kimila.

akizungumzia majukumu ya viongozi na taasisi za kiuongozi ndani ya kijiji katika kusimamia ardhi ya kijiji alisema kuwa halmashauri ya kijiji inawajibu  wa  Kupendekeza majina ya wanakijiji kwa ajili ya kuunda kamati za  uhakiki wa maslahi ya ardhi ya kijiji ambayo inaundwa na wajumbe wasiozidi 9 ambapo nusu yao lazima wawe wanawake. Kamati ya Mpango wa Matumizi bora ya ardhi inaundwa na wajumbe 8 ambapo wajumbe 3 lazima wawe wanawake

kwa upande wake  naibu afisa ardhi mshauri wa mradi huo MALAKI MSIGWA  alisema kuwa Awamu ya kwanza ya mradi imekamilika na LTA imefanikiwa kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Vijiji 36 kati ya vijiji 41 katika Wilaya za Iringa na Mbeya kwa gharama ya wastani wa dola 1800 za kimarekani.

Alisema kuwa mradi wa urasimishaji ardhi vijijini (LTA) unatekelezwa katika Wilaya za Iringa na Mbeya ili kuwezesha Halmashauri za wilaya katika kutoa huduma za umiliki wa ardhi chini ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Namba 5 ya mwaka 1999

Msigwa Alisema kuwa katika miaka minne ya kwanza ya utekelezaji, LTA iliwezesha kutambua na kusajili hakimiliki za kimila, kuwezesha upangaji wa matumizi ya ardhi za vijiji, na kuongeza uelewa wa utumiaji wa ardhi na haki za ardhi katika Wilaya za Iringa.

Aliongeza kuwa iliwezesha mpango kina wa makazi kwa vijiji vinne kwa gharama ya wastani ya dola 3500, uhakiki wa vipande vya ardhi zaidi ya 70,000 katika vijiji 41 na kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila zaidi ya 63,000 ambapo karibia asilimia 90 ya hati hizo zimechukuliwa na wamiliki.

Alisema kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa viongozi waandamizi wa Kata yana lengo la kuwajengea uelewa mpana kuhusua masuala ya usimamizi wa Ardhi na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi, ili haki iweze kutendeke kwa wananchi kwa kuzingatia utaratibu wa sheria zinazohusika na usimamizi na utawala wa Ardhi.

 Msigwa alisema kuwa kupitia mafunzo hayo wanategemea kama mradi kuongeza ufanisi wa kuratibu na kusimamia shughuli za Ardhi utaongezeka pamoja na kuongeza ushirikiano kwa wananchi serikali na viongozi wao.

Nao maafisa tarafa Yakub Kiwangwa wa IDODI na LUCY MGILWANGA Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiwele walisema kuwa Mpango wa urasimishaji Ardhi umesaidia kupunguza Migogoro ya ardhi katika maeneo.

Afisa wa uenezi wa mradi LTA Jackline Mhegi alisema  kuwa awamu ya pili ya mradi huo imejikita katika vijiji 70 vilivyobaki katika Halmashauri ya wilaya ya  Iringa inayofanyika kwa mfumo wa uchangiaji za gharama za upimaji na usajili wa ardhi katika vijiji, ambapo wamiliki wa ardhi watalazimika kuchangia kiasi cha TSH.30,000 kwa hati ya hakimiliki ya kimila, Kulingana na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na 5, ya mwaka 1999 na kanuni zake za mwaka 2001.

“Wananchi wanatakiwa kuchangia gharama za upimaji na usajili wa ardhi ili kumilikishwa ardhi zao kwa mujibu wa sheria kama vile ada ya maombi ya hakimiliki ya kimila, ada ya usajili na ada ya uhakiki wa maslahi ya ardhi” alisema Mhegi.

Alisema kuwa LTA inashirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Iringa pamoja na Halmashauri za vijiji katika kutekeleza shughuli za Kuhakiki mipaka ya ardhi ya vijiji na kuandaa vyeti vya ardhi vya vijiji, Kuandaa Mipango ya matumizi bora ya Ardhi, Kuhamashisha wananchi, Kuhakiki maslahi ya ardhi kwa mpangilio,Kuandaa na kusajili hati za hakimiliki za kimila .

Alisema kuwa Zoezi hili litafanyika kwa kutumia teknolojia ya simu ya mfumo wa (MAST) na kazi itafanywa na wanakijiji wenyewe kwa kushirikiana na wataalam kutoka wilayani na wengine kutoka katika mradi.

Naye Katibu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Avdensi Machenje amesema kuwa uwepo wa LTA umepelekea Vijiji Vingi kuwa na hati miliki ya maeneo yao na yanatumika.

Mpango huo wa Urasimishaji Ardhi Vijijini awamu ya pili katika Wilaya ya Iringa utawawezesha wanakijiji wenye vipande vya Ardhi kuchangia shilingi elfu 30 ili waweze kupata hati miliki za ardhi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com